Qatar yautaka Umoja wa Ulaya kuiwekea mashinikizo Saudi Arabia
Mkuu wa Kamati ya Taifa ya Haki za Binadamu ya Qatar ameuomba Umoja wa Ulaya kuiwekea mashinikizo zaidi Saudi Arabia ili iondoe vikwazo vyake dhidi ya Qatar.
Ali bin Samikh al Marri amesisitiza kwenye mahojiano na gazeti la Standard la nchini Austria kuwa: Raia wanne wa Qatar wametoweka nchini Saudi Arabia tangu kuanza mgogoro wa Qatar na kupasishwa vikwazo dhidi ya nchi hiyo. Al Marri ameashiria hatua ya Umoja wa Mataifa ya kuingilia kadhia hiyo na kuongeza kuwa, raia mmoja wa Qatar ameachiwa huru baada ya kufanya mazungumzo na Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa. Hata hivyo amesema raia wengine watatu wa Qatar wametoweka huko Saudi Arabia.
Saudi Arabia, Imarati, Bahrain na Misri zilikata uhusiano wao wa kidiplomasia na Qatar tarehe tano Juni mwaka jana zikiituhumu Doha kuwa inaunga mkono ugaidi na kufunga mipaka ya nchi kavu, baharini na anga baina ya nchi hizo na Qatar.
Nchi hizo ziliainisha masharti 13 kwa ajili ya kuanzisha tena uhusiano wao na Qatar ambapo kutekelezwa kila sharti miongoni mwao kunaweka alama ya kuuliza kuhusu mamlaka ya kujitawala nchi hiyo. Doha kwa upande wake ilipinga madai ya nchi hizo na kutangaza kuwa, hazina sababu yoyote yenye mashiko ya kuthibitisha madai hayo.