Kushadidishwa mzingiro wa Ghaza ni katika sera za kibaguzi za Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i50605-kushadidishwa_mzingiro_wa_ghaza_ni_katika_sera_za_kibaguzi_za_israel
Utawala wa Kizayuni wa Israel umekamilisha ujenzi wa ukuta wa kibaguzi baharini kaskazini mwa Ukanda wa Ghaza na hivyo kushadidisha mzingiro wa eneo hilo
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 03, 2019 04:50 UTC
  • Kushadidishwa mzingiro wa Ghaza ni katika sera za kibaguzi za Israel

Utawala wa Kizayuni wa Israel umekamilisha ujenzi wa ukuta wa kibaguzi baharini kaskazini mwa Ukanda wa Ghaza na hivyo kushadidisha mzingiro wa eneo hilo

Kanali ya 10 ya Televisheni ya Utawala wa Kizayuni wa Israel imetangaza kuwa, jeshi la utawala huo limekamilisha ujenzi wa ukuta wa katika mpaka wa baharini kaskazini mwa Ukanda wa Ghaza.

Gazeti la Al Quds al Arabi limeandika katika ripoti yake kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel umeuzingira Ukanda wa Ghaza kwa njia kadhaa ambazo ni mzingiro wa nchi kavu, baharini na angani. Gazeti hilo limeongeza kuwa, mzingiro huo ndio chanzo kikuu cha vifo vya Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza. Sera za utawala wake Kizayuni katika ujenzi wa ukuta baharini zimepelekea eneo hilo kutajwa kuwa ni 'eneo la mauti' kwa Wapalestina. Ripoti hiyo imeongeza kuwa: "Jeshi la Utawala wa Kizayuni wa Israel linajaribu kuhakikisha kuwa hakuna habari zinazoenea kuhusu eneo ambalo kumejengwa ukuta huo wa kibaguzi baharini. Eneo ambalo limejengwa ukuta huo lina upana  wa kuanzia mita 100 hadi 300. Kwa mujibu wa uchunguzi wa Umoja wa Mataifa eneo hilo ni asilimia 17 ya pwani ya Ukanda wa Ghaza. Aidha Umoja wa Matiafa unasema utawala wa Kizayuni wa Israel umeghusubu asilimia 35 ya ardhi za kilimo katika Ukanda wa Ghaza kwa ujenzi wa kizuizi hicho na hatua hiyo inahesabiwa kuwa miongoni mwa sera za kujitanua za utawala wa Kizayuni. Umoja wa Mataifa pia umesema ujenzi wa ukuta huo katika pwani ni jambo ambalo litazidisha masaibu ya kiuchumi na kuwafanya wakaazi wa Ghaza kuendelea kukosa makazi na kuwa wakimbizi."

Utawala haramu wa Israel umejenga ukuta huo mpya wa kibaguzi katika ardhi za Palestina katika hali ambayo Umoja wa Mataifa na taasisi za kimataifa za haki za binadamu zimeutaja ujenzi huo kuwa mbinu mpya ya ubaguzi ambayo ni ukiukwaji wa wazi wa sheria za kimataifa.

Utawala wa Kizayuni wa Israel unafuatilia malengo kadhaa katika ujenzi wa ukuta huo wa kibaguzi katika ardhi za Palestina ambazo umezikali wa kwa mabavu. Ujenzi wa ukuta huo unatokana na utambulisho wa kibaguzi wa utawala wa Kizayuni wa Israel ambao pia unakalia kwa mabavu mji mtakatifu wa Quds (Jerusalem). Jambo la kuzingatiwa hapa ni kuwa, ujenzi wa ukuta wa kibaguzi unaashiria mambo yanayozikutanisha pamoja tawala ambazo msingi wao ni ubaguzi wa rangi kuanzia utawala wa ubaguzi wa rangi wa makaburi wa Afrika Kusini, tawala za Kifashisti, utawala wa Kinazi na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Ukuta wa Kibaguzi katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan uliojengwa na utawala haramu wa Israel

Tawala za kibaguzi hufuatilia malengo kadhaa katika kuweka kuta za ubaguzi ikiwa ni pamoja na kujitanua na kueneza satwa ya kibeberu na pia kuhimiza ubaguzi.

Katika fremu hii, Jeshi la Utawala wa Kizayuni kwa muda wa miezi kadhaa sasa limekuwa likijenga ukuta mkubwa kwa kutumia seruji na majabali katika mpaka wa nchi kavu na baharini wa Ukanda wa Ghaza.

Utawala wa Kizayuni aidha katika miaka ya hivi karibuni umejenga kuta za kibaguzi katika mpaka na Misri, miinuko ya Golan ya Syria na pia katika sehemu na maeneo ambayo ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina zinapakana na Jordan na Lebanon.

Kwa mtazamo wa wakuu wa utawala wa Kizayuni ujenzi wa kuta za kibaguzi na ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni ni mbinu ya kuainisha mipaka ya utawala huo gahsibu.

Kushadidishwa mzingiro katika maeneo ya Wapalestina, na pia kusongeza mbele sera za kujitanua kupitia kunyakua zaidi ardhi za Palestina ni kati ya malengo maengine yanayofuatiliwa na Israel katika ujenzi wa kuta za kibaguzi. Wapalestina wamelaani vikali ujenzi mpya wa ukuta wa kibaguzi huko Ghaza.

Watoto ni waathirika wakubwa wa mzingiro wa utawala haramu wa Israel huko Ghaza

Kuwekwa ukuta mpya wa kibaguzi katika Ukanda wa Ghaza, eneo ambalo kwa miaka 12 sasa limekuwa chini ya mzingiro wa kinyama wa Israel ni jambo ambalo limewakasirisha waliwmengu. Jamii ya kimataifa inataka maafa ya Ghaza yasitishwe lakini utawala wa Kizayuni wa Israel 

chini ya himaya ya Marekani, umepuuza matakwa ya walimwengu na unaendelea ukandamizaji na udhalimu dhidi ya Wapalestina hasa katika Ukanda wa Ghaza.

Utawala wa Kizayuni unajaribu kuwafanya walimwengu wasahau kadhia ya Ghaza kwa kukata mawasiliano ya eneo hilo na dunia. Israel inaendeleza sera zake kadamizi katika eneo la Ghaza jambo ambalo litapelekea Wapalestina wakaazi wa eneo hilo kukumbwa na maafa makubwa ya kibinadamu katika mwaka huu wa 2019.