Jan 08, 2019 15:16 UTC
  • Saudia yawafukuza Waislamu wa Rohingya waliokimbia mauaji Myanmar

Saudi Arabia imewasafirishwa kwa nguvu hadi nchini Bangladesh makumi ya wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya waliotorokea nchini humo baada ya kushadidi mauaji na mashambulizi dhidi yao katika nchi yao ya Myanmar.

Shirika la habari la Middle East Eye limepokea kanda ya video inayowaonesha makumi ya wakimbizi hao katika Uwanja wa Ndege wa Jeddah, huku wametiwa pingu wakisubiri ndege ya kuwapeleka nchini Bangladesh.

Mmoja wa wakimbizi hao aliyerekodi video hiyo kwa kutumia simu ya mkononi anasema, wamekuwa wakizuiliwa katika jela ya Shumaisi mjini Jeddah kwa miaka mitano hadi sita, na sasa wanapelekwa kwa nguvu nchini Bangladesh.

Hii ni katika hali ambayo, hivi karibuni Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa aliitaka serikali ya Bangladesh kusimamisha shughuli ya kuwarejesha kwa nguvu nchini Myanmar maelfu ya wakimbizi Waislamu wa Rohingya, akisisitiza kuwa maisha yao yatakuwa hatarini katika nchi yao hiyo.

Wakimbizi Waislamu wa Rohingya nchini Bangladesh

Maelfu ya Waislamu wameuawa na wengine zaidi ya milioni moja wamelazimishwa kuwa wakimbizi ndani na nje ya Myanmar kutokana na mashambulizi yanayoendelea kufanywa na jeshi la nchi hiyo likishirikiana na Mabudha wenye misimamo mikali. 

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, jeshi la Myanmar limefanya mauaji ya kimbari dhidi ya jamii wa Waislamu wa nchi hiyo hususan katika jimbo la Rakhine.

Tags