Jan 09, 2019 09:31 UTC
  • Vibaraka 45 wa utawala wa Kizayuni watiwa mbaroni Ukanda wa Ghaza

Wizara ya Mambo ya Ndani na Usalama wa Taifa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) katika Ukanda wa Ghaza imetangaza habari ya kutiwa mbaroni raia 45 wa Palestina wanaotuhumiwa kushirikiana na kuufanyia ujasusi utawala haramu wa Israel.

Wizara hiyo inayosimamiwa na Hamas imetangaza kuwa, vibaraka hao wa utawala wa Kizayuni wametiwa mbaroni mashariki mwa mji wa Khan Yunis kusini mwa Ukanda wa Ghaza kuhusiana na faili la oparesheni iliyopewa jina la "Ncha ya Upanga."  Wizara hiyo imerusha hewani maelezo ya baadhi ya raia hao wa Kipalestina wakikiri kwamba walikuwa wakishirikiana na Israel na kuufanyia ujasusi utawala huo na kueleza kuwa vibara hao walitiwa mbaroni baada ya oparesheni ya mwezi Novemba mwaka jana ya timu maalumu za utawala wa Kizayuni  kusini mwa Ukanda wa Ghaza.  

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani na Usalama wa Taifa ya Hamas, Iyad al Bazm ametangaza baada ya kuonyeshwa baadhi ya mamluki hao wakikiri kushirikiana na Israel kwamba: Kitendo hicho kinadhihirisha kuwa, vibaraka wa maghasibu Wazayuni katika Ukanda wa Ghaza wapo mikononi mwa vyombo vya usalama vya Palestina na kwamba askari usalama watazima njama zao zote.

Iyad al Bazm, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani na Usalama wa Taifa ya Palestina inayosimamiwa na Hamas 
 

Itakumbukwa kuwa makomandoo kadhaa wa jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel mwezi Novemba mwaka jana walishambulia eneo la mashariki mwa mji wa Khan Yunis na kumuuwa shahidi mmoja wa makamanda wa ngazi ya juu wa Brigedi ya Shahidi Izzudin Qassam, tawi la kijeshi la harakati ya Hamas.  

  

Tags