Utawala haramu wa Israel, mlezi wa ugaidi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i51086-utawala_haramu_wa_israel_mlezi_wa_ugaidi
Kamanda wa jeshi la Lebanon ametangaza habari ya kutiwa mbaroni mamluki wa kigeni wa Shirika la Kijasusi la utawala haramu wa Israel (MOSSAD) ambaye alihusika katika jaribio la mauaji lililofeli dhidi ya Muhammad Omar Hamdan, mjumbe wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS katika mji wa Saida, Lebanon.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 24, 2019 08:56 UTC
  • Utawala haramu wa Israel, mlezi wa ugaidi

Kamanda wa jeshi la Lebanon ametangaza habari ya kutiwa mbaroni mamluki wa kigeni wa Shirika la Kijasusi la utawala haramu wa Israel (MOSSAD) ambaye alihusika katika jaribio la mauaji lililofeli dhidi ya Muhammad Omar Hamdan, mjumbe wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS katika mji wa Saida, Lebanon.

Gari la Muhammad Omar Hamdan, mjumbe wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS liliripuka Januari mwaka jana katika mji wa Saida Lebanon, hata hivyo kiongozi huyo wa Hamas alinusurika kifo katika shambulio hilo la kigaidi. Baada ya mwaka mmoja, jeshi la Lebanon limetangaza kuwa, limemtia mbaroni Hussein Ahmad Batu ambaye alihusika katika operesheni hiyo ya kigaidi. Gaidi huyo amekiri katika usaili aliofanyiwa kwamba, kuanzia mwaka 2014 hadi sasa amekuwa akifanya kazi na Shirika la Kijasusi la Israel (MOSSAD).

Kwa hakika kuna mfungaamano wa moja kwa moja baina ya Israel na ugaidi. Licha ya kuwa katika miaka ya hivi karibuni kwa kuibuka kundi la kigaidi la Daesh ambalo limetekeleza mashambuulio mbalimbali ya kigaidi barani Ulaya ugaidi umegeuka na kuwa tishio la dunia nzima, lakini kundi hilo na mfano wake yamefanya mambo ambayo hayana tofauti kabisa na yale yaliyofanywa na utawala haramu wa Israel. Tangu miongo kadhaa iliyopita, Israel imekuwa ikitekeleza operesheni za kigaidi dhidi ya wapinzani wake ikiwemo Lebanon, Palestina na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. 

Shirika la Kijasusi la Israel (MOSSAD)

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepoteza raia wake zaidi ya 17,000 waliouawa shahidi katika mashambulio ya kigaidi ambayo aghalabu yalifanyika nchini Iran katika miaka ya awali ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na Israel ilikuwa na mkono katika operesheni hizo za kigaidi. Shirika la Kijasusi la Israel (MOSSAD) limekuwa likiwanunua na kuwaajiri mamluki katika nchi mbalimbali na kuwapatia mafunzo kwa ajili ya kuwatumia katika operesheni mbalimbali za kigaidi.

Hatam Shalghoum wakili wa Muhammad al-Zouari alitangaza mwezi Mei mwaka jana kwamba, Zouari aliuawa na watu wawili waliokuwa wameajiriwa na Shirika la Kijasusi la Israel (MOSSAD(). Muhammad al-Zouari mhandisi wa ndege wa Tunisia alikuwa mjumbe wa Brigedi ya Izzuddin Qassam Tawi la Kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) ambaye aliuawa Disemba 2016 huko nchini Tunisia. Kuna mifano mingi inayoonyesha mamluki wa Israel wakikiri kuhusika katika operesheni za kigaidi.  Katika kipindi cha miongo mitatu pekee, Shirika la Kijasusi la Israel (MOSSAD) limetekeleza operesheni 14 za kigaidi dhidi ya viongozi wa Kipalestina na wa nchi nyingine za Kiarabu ambapo shakhsia 16 wa Kipalestina na Kiarabu wameuawa shahidi katika nchi 11 za Kiarabu na zisizo za Kiarabu katika operesheni hizo.

Kanali ya Pili ya Televisheni ya Israel hivi karibuni na  kwa mara ya kwanza  ilikiri katika moja ya vipindi vyake juu ya kuweko kikosi maalumu cha mauaji ndani ya Shirika la Kijasusi la Israel (MOSSAD) na kusema kuwa, kikosi hicho kimeshiriki katika makumi ya operesheni za mauaji katika maeneo mbalimbali ulimwengini ikiwemo nchini Iran.

Jeshi la Israel limekuwa likitenda jinai kila uchao dhidi ya Wapalestina

Hatua ya Israel ya kuwalenga viongozi, wajumbe wa makundi ya kisiasa na wasomi wa nchi mbalimbali  ni misdaqi na mfano wa wazi wa 'ugaidi wa kiserikali'. Kubobea Israel katika kuwanunua na kuwaajiri mamluki wa nchi mbalimbali na kisha kuwalea na kuwanadaa kwa ajili ya kuwatumia katika operesheni za kigaidi kabla ya kila kitu, sababu yake ni kuwa kimsingi Israel imeundwa kutokana na makundi ya kigaidi kama Mossad, Shabak, Shin Bet na makundi ya mauaji.

Licha ya Israel kuwa na faili jeusi kama hili, lakini utawala huo ghasibu umekuwa ukizituhumu nchi nyingine ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na baadhi ya harakati za kisiasa katika eneo la Mashariki ya Kati kama Hizbullah ya Lebanon na Hamas ya Palestina kwamba, zinajihusisha na vitendo vya kigaidi, tuhuma ambazo zimekuwa zikishikiwa bango na washirika wake kutokana na siasa za upande mmoja za Marekani kuwa na satua na uthibiti katika mfumo wa kimataifa na hivyo kupelekea kutofuatiliwa jinai  za utawala huo haramu.