Harakati za Israel za kushadidisha jinai katika maeneo ya Wapalestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i51305-harakati_za_israel_za_kushadidisha_jinai_katika_maeneo_ya_wapalestina
Baada ya utawala haramu wa Israel kulitimua kutoka katika mji wa al-Khalil huko katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kundi la waangalizi wa kimataifa, Kuwait imelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuitisha kikao cha dharura kuhusiana na kadhia hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 03, 2019 09:24 UTC
  • Harakati za Israel za kushadidisha jinai katika maeneo ya Wapalestina

Baada ya utawala haramu wa Israel kulitimua kutoka katika mji wa al-Khalil huko katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kundi la waangalizi wa kimataifa, Kuwait imelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuitisha kikao cha dharura kuhusiana na kadhia hiyo.

Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala ghasibu wa Israel hivi karibuni alikataa kuongezwa muda wa timu ya muda ya waangalizi wa Umoja wa Mataifa huko katika mji wa al-Khalil ulioko katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Baada ya kuuawa waumini 30  wa Kipalestina waliokuwa wakitekeleza ibada ya Swala katika Msikiti wa Ibrahim huko al-Khalil 1994, mauaji yaliyofanywa na Baruch Goldstein Mzayuni mwenye misimamo mikali, waangalizi wa kimataifa waliojulikana kwa jina la Temporary International Presence in Hebron (TIPH) walipelekwa katika mji wa al-Khalil.  Jukumu la waangalizi hao lilikuwa ni kuandaa ripoti kuhusiana na visa vya ukiukaji wa haki za binadamu na haki za mashirika ya kimataifa ya masuala ya kibinadamu katika mji huo.

Gazeti la al-Quds al-Arabi limeandika: Timu ya Kimataifa ya Umoja wa Mataifa katika mji wa al-Khalil imetekeleza majukumu yake kuhusiana na kuwahami Wapalestina na kwa msingi huo kuendelea kuweko timu hiyo katika mji huo ni jambo la dharura na jamii ya kimataifa inapaswa kufanya hima kutoruhusu mauaji  ya Goldstein yakaririwe tena.

Wapalestina wakiandamana kulalamikia hatua ya Benjamin Netanyahu ya kukataa kuwaongezea muda wasimamizi wa kimataifa katika mji wa al-Khalil

Kwa msingi huo, utawala haramu wa Israel umezusha propaganda mbalimbali ukiwemo mwenendo wa mapatano na kufanya ukwamishaji mambo katika njia ya shughuli za wasimamizi wa kimataifa, ambapo kwa kupinga kuweko wanaharakati hao au kuzuia kupanuliwa shughuli zao katika maeneo ya Wapalestina, umejiandalia mazingira ya kudumisha na kushadidisha jinai zake dhidi ya Wapalestina.

Katika anga isiyo tulivu na ya utumiaji mabavu ambayo imeletwa na Israel katika ardhi za Palestina, waangalizi wa kimataifa na walinda amani wa Umoja wa Mataifa wana nafasi muhimu ya kufichua jinai za utawala huo ghasibu. Inaonekana kuwa, sababu ya kwanza ya uamuzi wa Benjamin Netanyahu ni ripoti ndefu ya kamati hiyo ya uangalizi ya kimataifa huko katika mji wa al-Khalil ambayo imesajili zaidi ya matukio 4,000 ya ukiukaji wa haki za binadamu uliofanywa na Israel. Aidha timu hiyo ya Umoja wa Mataifa imechunguza madai ya walowezi wa Kizayuni kwamba, wana hati miliki za ardhi huko al-Khalil za mwaka 1929 na kutupilia mbali madai hayo.

Fauka ya hayo,ripoti ya timu hiyo ya Umoja wa Mataifa imeeleza kinagaubaga kwamba, ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni sio halali kwa mujibu wa sheria za kimataifa. Kwa msingi huo inaonekana kuwa, uamuzi wa Benjamin Netanyahu wa kukataa kuongeza muda wa kubakia timu hiyyo ya Umoja wa Mataifa huko al-Khalil unalenga kuwakomoa wajumbe wa timu hiyo kutokana na kuandaa ripoti ya ufichuaji dhidi ya Israel.

Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala bandia wa Israel

Aidha Netanyahu anakusudia kulitumia suala hilo kisiasa ili kuwavutia wafuasi wa mrengo wa kushoto wenye misimamo mikali na walowezi wa Kizayuni ambao tangu awali wamekuwa wakipinga shughuli za timu hiyo hususan katika mji wa al-Khalil. Kwa kuzingatia kukaribia kufanyika uchaguzi wa Bunge wa Israel wa kabla ya wakati na kesi zinazomkabili Netanyahu hususan mafaili ya ufisadi, ni jambo lililo wazi kwamba, hatua hiyo ya Nentanyahu kabla ya kitu kingine ina malengo ya kisiasa. Katika anga na mazingira kama haya, ilikuwa ikitarajiwa kwamba, Netanyahu angeizima sauti yoyote ile ambayo inalenga kufichua hatua za kivamizi na ujenzi wa vitongoji vya walowezi unaofanywa na utawala huo ghasibu na hivyo kukiuka mikataba na maazimio yote ya kimataifa. 

Israel kutokana na kuhofia kufichuliwa zaidi jinai zake ambapo litakalofuata ni kufuatiliwa kimataifa jinai hizo, daima imekuwa ikikwamisha shughuli za wawakilishi wa Umoja wa Mataifa na wajumbe wa kamati za kimataifa ambapo awali huwabambikizia tuhuma na hivyo kuzuia shughuli zao. Miamala hii ya Israel inazidi kuweka wazi utambulisho ulio dhidi ya amani na ukiukaji wa sheria za kimataifa wa utawala huo. Hapana shaka kuwa, ni jambo la dharura kwa jamii ya kimataifa hususan Umoja wa Mataifa kuuchukulia hatua utawala huo ambao umehatarisha amani na uthabiti wa kimataifa.