Vita katika nchi za Kiarabu vyagharimu dola bilioni 900
Benki ya Dunia imekadiria gharama ya kuendeshea vita katika nchi za Kiarabu katika miaka minane iliyopita kuwa dola bilioni 900.
Harakati za mapinduzi ya wananchi katika nchi za Kiarabu pia zinapitisha mwaka wake wa tisa sasa, ambapo zilitazamiwa kupelekea kuasisiwa tawala za kidemokrasia katika nchi hizo hata hivyo zimeibua na kueneza vitendo vya mabavu na machafuko katika kalibu mbalimbali vikiwemo vita vya wenyewe kwa wenyewe na baina ya nchi na nchi. Zaidi ya yote, maslahi ya baadhi ya madola ya eneo la Asia Magharibi na yale ya mbali yamekuwa chanzo cha kubadilika mwenendo wa harakati za mapambano ya wananchi katika nchi hizo za Kiarabu kutoka demokrasia kuelekea kwenye machafuko na vita. Vita kati ya serikali ya Syria na magaidi wanaoungwa mkono na muungano wa nchi za Kiarabu, utawala wa Kizayuni na nchi za Magharibi, vita vya muungano vamizi wa Saudia dhidi ya Yemen, vita vya ndani huko Libya na vile vya Iraq na magaidi wa Daesh ni miongoni mwa vita muhimu zaidi vilivyoshuhudiwa miaka minane iliyopita katika ulimwengu wa Kiarabu.
Mshindi mkuu wa vita hivyo ni utawala wa Kizayuni ambayo ina maslahi katika katika mapigano, vita vya ndani na vile vinavyojiri kati ya nchi za Kiislamu. Utawala wa Kizayuni ambao mwaka 2011 uliingiwa na wasiwasi na hofu kutokana na kupamba moto kwa harakati hizo za mapinduzi za wananchi katika nchi za Kiarabu na kujiona ukiwa imetengwa zaidi katika Mashariki ya Kati sasa imejielekeza katika kuhuisha uhusiano wake na nchi za Kiarabu baada ya harakati hizo za mapinduzi kugeuka na kuwa za machafuko, na baadhi ya tawala za Kiarabu kushindwa kumtambua vyema adui. Utawala wa Kizayuni aidha unaunga mkono kushtadi hali ya mchafukoge, ukosefu wa amani, vita na mapigano ya wenyewe kwa wenye na kati ya nchi za Kiislamu.
Katika upande wa pili, mshindwa mkuu wa vita hivyo ni wananchi, serikali za nchi zinazopigana vita na pia tawala zinazosababisha vita. Bila shaka wananchi ndio washindwa wa vita hivyo kwa sababu vita hivyo vimesababisha maelfu ya raia kuuawa, mamia ya maelfu kujeruhiwa na makumi ya mamilioni kuwa wakimbizi. Mfano wa wazi wa kushindwa huko ni kuharibiwa na kubomolewa miundo mbinu ya maisha ya mamilioni ya raia wa Syria,Yemen, Iraq na Libya katika vita hivyo; huku raia wa nchi hizo wakifanya juhudi ili kubaki hai na si kwa ajili ya kuendesha maisha. Serikali za nchi panakojiri vita ni washindwa wa vita hivyo kwa sababu mosi tawala hizo zimekabiliwa na uingiliaji wa nchi ajinabu na hazina nguvu tena kama ilivyokuwa kabla ya mwaka 2011. Pili ni kuwa, miundo mbinu katika miji ya nchi hizo zilizoathiriwa na vita imesambaratika na mabilioni ya dola yanahitajika kwa ajili ya ujenzi mpya na ukarabati. Tatu ni kuwa, ukarabati unahitajika katika nchi hizo kwa kuzingatia madhara ya kiusalama yaliyozisibu nchi hizo. Wakati huo huo nchi zilizoanzisha vita nazo pia ni miongoni mwa washindwa wa vita hivyo kwa sababu zimetumia kiasi kikubwa cha pesa vitani kwa kukimbilia kuanzisha vita na uvamizi katika nchi nyingine badala ya kustafidi na maliasili za nchi hizo kwa ajili ya kuimarisha miundo mbinu katika sekta za afya, elimu na sayansi.
Kwa msingi huo, hata nchi kama Saudi Arabia ambazo siku zote zimekuwa na bajeti ya ziada nazo pia zimekabiliwa na nakisi ya bajeti.
Mohammed bin Abdullah Waziri wa Fedha wa Saudi Arabia mwishoni mwa Septemba mwaka jana alitangaza kuwa bajeti ya nchi hiyo mwaka 2019 itafika dola bilioni 34. Ni wazi kuwa fedha nyingi zinahitajika kwa ajili ya ujenzi mpya katika nchi zilizoathiriwa na vita. Muhammad Muhyiddin Makamu wa Kwanza wa Mkuu wa Benki ya Dunia anasema: Hasara za uharibifu na kupotea fursa za maendeleo na ustawi katika nchi za Kiarabu zilizokumbwa na vita katika miaka ya kuanzia 2010 hadi mwaka jana 2018 zimefika dola bilioni 900.
Hii ni katika hali ambayo maafisa wengine wa Benki ya Dunia wamekitaja kiwango hicho cha hasara kuwa cha chini sana na wanaamini kuwa vita hivyo vimezigharimu pakubwa nchi za Kiarabu.