Afrika Kusini yalaani ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni
Serikali ya Afrika Kusini imelaani kuendelea ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel.
Harshana Goolab, Katibu wa Kwanza wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni na Ushirikiano wa Kimataifa ya Afrika Kusini amesema hayo katika kikao cha Baraza la Uusalama la Umoja wa Mataifa kilichoitishwa kujadili kadhia ya Palestina na Masharikki ya Kati na kusema kuwa, kujengwa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu likiwemo eneo la Quds Mashariki ni kukiuka wazi sheria za kimataifa.
Harshana Goolab amelaani vikali jinai za utawala dhalimu wa Israel katika maandamano ya "Haki ya Kurejea" na kutoa wito wa kuchukuliwa hatua za kukomeshwa jinai hizo za Wazayuni dhidi ya Wapalestina.
Kadhalika Katibu wa Kwanza wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni na Ushirikiano wa Kimataifa ya Afrika Kusini amekosoa vikali hatua ya Rais Donald Trump wa Marekani ya kutambua rasmi umiliki na udhibiti wa Israel kwa miinuko ya Golan ambayo ni mali ya Syria.
Ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi ya Palestina unafanyika kwa shabaha ya kubadili muundo wa kijamii na kijiografia wa ardhi ya Palestina.
Maafisa mbalimbali wa Umoja wa Mataifa na mashirika ya kieneo na kimataifa ya kutetetea haki za binadamu yamekuwa yakisisitiza kwamba, kwa mujibu wa sheria za kimataifa, ujenzi wa vitongoji vya walowezi unaofanywa na Israel katika ardhi unazozikalia kwa mabavu za Palestina ni kinyume cha sheria na inapaswa usimamishwe kikamilifu.