Apr 18, 2016 14:35 UTC
  • Mazungumzo ya amani ya Yemen yaakhirishwa

Pande zinazopigana nchini Yemen zimetangaza kuwa mazungumzo ya amani ya nchi hiyo yameakhirishwa.

Viongozi wa pande hizo hasimu wamesema mazungumzo hayo yaliyokuwa yamepangwa kufanyika leo nchini Kuwait yameakhirishwa.

Wawakilishi wa ujumbe wa harakati ya Ansarullah wamesema kutokana na kuendelea kukiukwa usitishaji vita kunakofanywa na muungano unaoongozwa na Saudi Arabia hawatoelekea Kuwait kushiriki mazungumzo hayo.

Ripoti zinaeleza kuwa japokuwa mazungumzo ya kusaka amani nchini Yemen yalipangwa kuanza leo, lakini jumbe za harakati ya Ansarullah na chama cha Kongresi ya Wananchi bado hazijaondoka Yemen kuelekea Kuwait na wala haijaelezwa mazungumzo hayo yatafanyika lini.

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen Ismail Ould Sheikh Ahmed, ametahadhrisha juu ya taathira hasi za ukiukaji makubaliano ya usitishaji vita ulioanza kutekelezwa tarehe 11 mwezi huu.

Mazungumzo ya leo nchini Kuwait yalikuwa yashirikishe pande zinazopigana nchini Yemen ukiwemo ujumbe wa harakati ya muqawama wa wananchi ya Ansarullah na ule wa rais wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kuitoroka nchi Abd Rabbuh Mansur Hadi.

Duru iliyopita ya mazungumzo hayo iliyofanyika mjini Geneva, Uswisi ilimalizika bila ya kuwa na tija.../

Tags