Jun 14, 2019 02:26 UTC
  • Dada yake Bin Salman kufikishwa katika mahakama ya jinai Ufaransa

Dada yake Mohammad Bin Salman, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia anatazamiwa kupandishwa kizimbani mwezi ujao wa Julai katika mahakama ya jinai nchini Ufaransa, akiandamwa na shitaka la kumuagiza mlinzi wake kumpiga mfanyakazi wa kiume mjini Paris.

Duru za habari zimeliambia shirika la habari la AFP kuwa, bintimfalme Hassa bint Salman atashitakiwa mwezi ujao nchini Ufaransa, kwa kutoa agizo la kushambuliwa fundi bomba katika jumba lake la kifahari mjini Paris mnamo mwezi Septemba mwaka 2016.

Fundi huyo ambaye alikuwa amekodishwa kwa ajili ya kufanya marekebisho kwenye jumba la bintimfalme huyo wa Saudia anaripotiwa kupiga picha chumba ambacho alitakiwa akifanyie ukarabati, ndipo dadake Bin Salman akamuagiza mlinzi wake ampe kichapo cha mbwa, akimtuhumu kuwa alitaka kwenda kuuza picha hizo kwa waandishi wa habari.

Gazeti la Ufaransa la Le Point limenukuu simulizi ya tukio hilo kutoka kwa kijana huyo aliyeshambuliwa, ambaye amesema mbali na kutandikwa vibaya lakini pia binti huyo wa Mfalme wa Saudia alimtukana matusi mabaya.

Maandamano ya kulaani mauaji ya Khashoggi

Amesema miongoni mwa cheche za maneno makali alizorushiwa na Hassa bint Salman ni, "Lazima tumuue huyo mbwa, hapaswi kuendelea kuishi." Fundi huyo alijeruhiwa vibaya kiasi cha kushindwa kuripoti tena kazini mwa siku kadhaa.

Familia ya Aal-Saud ni mashuhuri kwa ukatili na udhalilishaji. Tarehe pili Oktoba 2018, maafisa 15 wa serikali ya Saudi Arabia walitumwa mjini Istanbul Uturuki kutokea Riyadh kwenda kumuua mwandishi mmoja wa habari aliyekuwa anaukosoa utawala wa hivi sasa wa Saudia, Jamal Khashoggi kwa amri ya Bin Salman.

 

 

 

Tags