Saudia yanunua programu ya kijasusi ya Israel kwa dola milioni 300
Saudi Arabia imeripotiwa kununua programu ya kufanya ujasusi yenye thamani ya dola milioni 300 kutoka utawala wa Kizayuni wa Israel.
Hayo yamefichuliwa na tovuti ya habari ya al-Khaleej ambayo imeongeza kuwa, utawala wa Riyadh unatumia programu hiyo ya kijasusi ya kudukua kompyuta au simu za mkononi (spyware) kuwafanyia ujasusi viongozi wa upinzani na wakosoaji wa utawala huo wa kifalme.
Kwa mujibu wa tovuti hiyo, wawakilishi wa Riyadh bila ya uwepo wa mpatanishi walikutana moja kwa moja na mashirika ya kijasusi ya Israel mjini London, Uingereza mwishoni mwa mwezi Mei, na kusaini mauzo ya programu hiyo ya kuwafuatilia wakosoaji wake. Hivi karibuni, gazeti la Kizayuni la Haaretz liliripoti kuwa, Saudi Arabia, Bahrain na Imarati (UAE) zina mikataba mikubwa sana ya kununua vifaa vya kijasusi kutoka kwa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Itakumbukwa kuwa, shirika moja la kijasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel lilitoa msaada mkubwa kwa ufalme Saudi Arabia ili kufanikisha mauaji ya mwandishi habari Jamal Khashoggi ambaye alikuwa mkosoaji mkubwa wa ufalme huo wa kiimla.
Hayo yalifichuliwa na gazeti la New York Times ambalo liliandika mwishoni mwa mwaja jana kuwa, shirika hilo la ujasusi wa mitandaoni la Israel la NSO Group lilitumika katika kufuatilia mawasiliano ya simu ya Khashoggi na kuwakabidhi wakuu wa Saudia taarifa zote za mawasiliano ya mwandishi huyo ambaye aliuawa kinyama kwenye jengo la ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul, Uturuki mnamo tarehe Pili Oktoba kwa jana.