Zarif asisitiza umuhimu wa kuzingatia kadhia ya wakimbizi wa Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i547-zarif_asisitiza_umuhimu_wa_kuzingatia_kadhia_ya_wakimbizi_wa_syria
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ametaka kuzingatiwa kadhia ya wakimbizi wa Syria na hali ngumu ya kibinadamu nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 04, 2016 03:23 UTC
  • Zarif asisitiza umuhimu wa kuzingatia kadhia ya wakimbizi wa Syria

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ametaka kuzingatiwa kadhia ya wakimbizi wa Syria na hali ngumu ya kibinadamu nchini humo.

Muhammad Jawad Zarif ambaye ameelekea Uingereza kwa lengo la kushiriki kwenye kikao cha kiataifa cha kuwasaidia wananchi wa Syria alisema jana usiku katika mkutano na waandishi wa habari wakati alipowasili mjini London kuwa mkutano wa kuisaidia Syria ni fursa kwa ajili ya kubainisha misimamo ya Tehran kuhusiana na mgogoro wa nchi hiyo. Zarif ameongeza kuwa atakutana na kufanya mazungumzo na baadhi ya washiriki wa mkutano huo na vilevile viongozi wa Uingereza na wa taasisi za utafiti za nchi hiyo pambizoni mwa mkutano huo wa kimataifa kuhusu Syria.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameeleza kuwa watatumia fursa iliyopatikana kwa ajili ya kuchunguza njia bora ya kutekeleza makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1 na vilevile kuchunguza hali ya mambo katika eneo la Mashariki ya Kati hususan Syria na Yemen.

Kikao cha kimataifa cha kuwasaidia wananchi wa Syria kinafunguliwa leo Alhamisi huko London, Uingereza. Kikao hicho kinahudhuriwa na marais wa nchi, taasisi za kimataifa, mashirika yasiyo ya kiserikali na yale ya binafsi kutoka nchi zaidi ya 70.