Utawala wa Bahrain unapanga mikakai ya kuwafuta kazi walimu wa Kishia
(last modified Mon, 26 Aug 2019 12:02:16 GMT )
Aug 26, 2019 12:02 UTC
  • Utawala wa Bahrain unapanga mikakai ya kuwafuta kazi walimu wa Kishia

Duru za habari nchini Bahrain zimeripoti kuwa, utawala wa Aal Khalifa nchini humo unapanga mikakati ya kuwatimua maelfu ya walimu Waislamu wa madhehebu ya Shia wa nchi hiyo.

Ripoti zinasema kuwa, utawala wa Bahrain unafanya jitihada za kuajiri idadi kubwa ya waalimu kutoka Saudi Arabia na Misri na kuwaingiza katika mfumo wa elimu wa nchi hiyo.

Katika siku za hivi karibuni utawala wa Aal Khalifa umewaajiri walimu wengi kutoka nchi za Saudi Arabia na Misri na kwamba maelfu ya walimu wa Bahrain waliokuwa wakisubiri kusajiliwa kwa ajili ya kuchukua nafasi hizo wamepuuzwa na kunyimwa ajira kwa sababu tu ni Waislamu wa madhehebu ya Shia. Ni vyema kukumbusha hapa kuwa, asilimia kubwa ya jamii ya watu wa Bahrain inaundwa na Waislamu wa Shia. 

Jumuiya ya al Wifaq ya Bahrain imelaani hatua hiyo ya utawala wa Aal Khalifa na kutangaza kuwa, serikali ya Manama ndiyo inayopaswa kuwajibishwa kutokana na uamuzi huo unaochochewa na chuki za kimadhehebu.

Waislamu wengi wa madhehebu ya Shia wa Bahrain wamefungwa jela au kunyongwa

Taarifa iliyotolewa na al Wifaq imesema kuwa, hatua hiyo ya Wizara ya Elimu ni mpango unaotaka kuzusha fitina na uharibifu katika jamii, na uamuzi kama huo mkubwa hauwezi kuchukuliwa na waziri au afisa yeyote mwingine isipokuwa viongozi wa juu wa utawala wa Aal Khalifa. 

Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Bahrain wamo katika kipindi kigumu sana na hadi sasa mamia miongoni mwao wamepokonywa uraia wao, kunyongwa au kufungwa jela.