Amnesty International yaikosoa Ufaransa kwa kuendelea kuziuzia silaha Saudia na Imarati
Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International limeikosoa vikali serikali ya Ufaransa kutokana na hatua yake ya kuendelea kuziuzia silaha Saudi Arabia na Imarati.
Taarifa ya Amnestry International sambamba na kuikosoa hatua hiyo ya Ufaransa imeitaka serikali ya Paris isitishe mara moja kuziuzia silaha nchi hizo mbili za Kiarabu zinazohusika pakubwa katika vita vya Yemen.
Kadhalika taarifa hiyo imeeleza kuwa, inasikitisha kuona kwamba, licha ya kuweko uwezekano mkubwa wa silaha za Ufaransa inazoziuza kwa Saudi Arabia na Imarati kutumiwa katika mauaji dhidi ya watoto wa Yemen, lakini Paris imeendelea kuziuza silaha zake kwa nchi mbili hizo.
Aidha Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International mbali na Ufaransa, imezitaja pia Marekani, Uingereza, Uhispania na Canada kwamba, zimeendelea kuipatia silaha Saudi Arabia na Imarati, licha ya Riyadh kuongoza muungano wa kijeshi dhidi ya Yemen.

Hayo yanajiri katika hali ambayo ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa, Saudi Arabia ni mnunuzi mkubwa kabisa wa silaha za madola ya Magharibi na kwa mwaka hutumia mamilioni ya dola kwa ajili ya kununua silaha na tangu ilipoivamia kijeshi Yemen, imekuwa ikitumia silaha hizo dhidi ya watoto, wanawake na wazee wa nchi hiyo wasio na hatia.
Umoja wa Mataifa umevitaja vita vya Yemen ambavyo hadi sasa vimepelekea maelfu ya watu kuuawa na mamilioni ya wengine kukabiliwa na baa la njaa kuwa, 'mgogoro mbaya zaidi wa kibinadamu ulimwenguni."