Uturuki kuanzisha vyuo vitatu kaskazini mwa Syria
Vyombo vya habari vya Uturuki vimeripoti juu ya uamuzi wa serikali ya Rais Recep Tayyip Erdoğan wa nchi hiyo wa kuanzisha vyuo vitatu, huko kaskazini mwa Syria, chini ya usimamizi wa Chuo Kikuu cha Gaziantep cha Uturuki.
Vyombo hivyo vya habari vimearifu kwamba Chuo kikuu cha Gaziantep kinakusudia kufungua chuo cha taaluma ya uchumi na masuala ya idara katika mji wa Al Bab, chuo cha elimu ya Kiislamu katika mji wa Azaz na chuo cha taaluma ya malezi katika mji wa Afrin, kaskazini mwa Syria. Mwezi Disemba mwaka jana, pia serikali ya Rais Recep Tayyip Erdoğan ilichukua hatua ya kuanzisha baraza la makabila ya vijijini nchini Syria. Kabla ya hapo pia viongozi wa serikali ya Erdogan sambamba na kuainisha wakuu wa mikoa wa maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya Syria, walijaribu pia kueneza utawala wao ndani ya maeneo ya nchi hiyo jirani ya Kiarabu. Matukio hayo yanajiri katika hali ambayo serikali ya Syria haina uwezo wa kulinda ardhi yake yote, kutokana na mashinikizo ya madola ya Mgharibi na baadhi ya tawala tegemezi za eneo la Ghuba ya Uajemi. Kwa hakika hatua hiyo ya Uturuki inachochea na kuvuruga hali ya mambo nchini Syria. Katika miaka ya hivi karibuni serikali ya Rais Recep Tayyip Erdoğan imezikalia kwa mabavu baadhi ya ardhi za Syria.
Mkabala wake viongozi wa serikali ya Damascus, daima wamekuwa wakilaani vikali kitendo cha kukaliwa kwa mabavu ardhi ya nchi hiyo kunakofanywa na askari wa Uturuki na Marekani, kama ambavyo wamekuwa wakitaka kuondoka askari hao nchini humo. Viongozi wa serikali ya Erdoğan wanazungumzia kuanzisha vyuo vyao kaskazini mwa Syria, katika hali ambayo siku zote hizi wamekuwa wakidai kuwa, sababu ya kuivamia kijeshi nchi hiyo ya Kiarabu, ni kupambana tu na makundi ya kigaidi hususan kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS). Licha ya kueneza propaganda kuhusiana na suala hilo, lakini kile kinachoonekana ni njama ya serikali ya Ankara ya kutaka kubakia kwa muda mrefu zaidi ndani ya Syria. Katika uwanja huo tunaweza kusema kuwa, ni wazi kwamba serikali ya Rais Recep Tayyip Erdoğan haijafungamana hata na makubaliano iliyoafikiana na Iran na Russia kuhusiana na Syria. Katika mazingira hayo, ni suala lililo mbali kuwa askari wa Uturuki watafikia malengo yao kwa urahisi ndani ya Syria. Kuhusiana na jambo hilo Mohammad Shahin, Naibu Katibu Mkuu wa Baraza la Utendaji katika eneo la mashariki mwa Mto Furati la upande wa Kurdistan ambaye pia ni mtaalamu wa masuala ya kisiasa ya Syria akizungumza na Shirika la Habari la Hawar, ameashiria vitisho vya hivi karibuni vya serikali ya Uturuki dhidi ya eneo hilo kwa kusema: "Hii sio mara ya kwanza kwa serikali ya Uturuki kutoa vitisho dhidi ya eneo hilo. Lengo la Erdoğan ni kulidhibiti kikamilifu eneo sambamba na kochochea zaidi mgogoro wa Syria. Mpango wa Uturuki wa kuasisi 'eneo salama' ni utangulizi wa kutaka kulidhibiti eneo lote. Iwapo rais huyo atafanikiwa kupata mazingira ya kuasisi eneo hilo la salama, basi eneo lote lijitayarishe kudhibitiwa na Ankara. Lengo kuu la Uturuki ni hilo. Uturuki pia imefanya hivyo katika maeneo ya Idlib, Afrin, Al Bab, A'zaz na Jarabulus."
Kwa kuzingatia msimamo na mtazamo wa Wakurdi wa Syria kuhusiana na vitisho vya serikali ya Rais Recep Tayyip Erdoğan tunaweza kusema kuwa, juhudi za Uturuki za kuanzisha vyuo vyake vitatu huko kaskazini mwa Syria si tu kwamba hazitakuwa na msaada wowote kwa wakazi wa maeneo hayo na hata serikali ya Damascus, bali zina maana ya kuendelea kubakia kwa muda mrefu zaidi serikali ya Ankara ndani ya maeneo hayo na kisha kutekeleza mipango ya kubadili muundo wa kijamii wa eneo na kisha kuyatawala kwa muda mrefu meneo ya kaskazini mwa Syria na mashariki mwa Mto Furati. Wakati huo huo tunaweza kusema kuwa licha ya matamshi ya rais wa Uturuki ya kutozikodolea macho ardhi za Syria na kuigawa nchi hiyo, lakini harakati za serikali yake zinaonyesha wazi kwamba, Ankara haina nia yoyote ya kuondoka nchini Syria hivi karibuni.