Vyombo vya habari vyafichua, Marekani inapeleka silaha kwa siri huko Yemen
Vyombo vya habari vimefichua kwamba, wiki iliyopita zana na silaha za kivita za Marekani ziliingizwa kusini mwa Yemen zikibebwa na meli ya Saudi Arabia.
Televisheni ya CNN ya Marekani imerusha hewani mkanda wa video uliochukuliwa kwa siri unaoonesha magari ya deraya aina ya Oshkosh na silaha nyingine zilizotengenezwa Marekani zikipakuliwa katika bandari ya Aden kusini mwa Yemen.
Ikinukuu watu waliotoa ripoti hiyo ya siri na nyaraka za bandari ya Aden, televisheni ya CNN imeripoti kuwa, meli ya Saudi Arabia iliyopeleka silaha hizo za Marekani huko Yemen inaitwa Bahri Hofuf.
Nyaraka zilizopatikana zinaonesha kuwa, meli hiyo ilizima mfumo wake wa baharini kabla ya kuonekana katika bandari ya Aden tarehe 29 Oktoba.
Ripoti ya televisheni ya CNN inasema kuwa, vibaraka wa Saudi Arabia huko kusini mwa Yemen wanamtia nguvuni mtu yeyote anayeshukiwa kuwa ndiye aliyevujisha video ya kuwasili meli hiyo iliyokuwa na silaha za Marekani katika bandari ya Aden.
Saudi Arabia ikishirikiana na Marekani, Imarati, utawala haramu wa Israel na nchi nyingine kadhaa ilianzisha mashambulizi makali dhidi ya Yemen mwezi Machi 2015 sambamba na kuizingira nchi hiyo ya Kiarabu katika pande tatu za nchi kavu, angani na baharini. Hadi sasa vita hivyo vimepelekea watu laki moja kuuawa na makumi ya maelfu ya wengine kujeruhiwa. Vilevile mamilioni ya Wayemen wamekuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi hiyo.