Mfumo wa ulinzi wa Syria watungua makombora ya Israel
Mfumo wa ngao ya ulinzi ya jeshi la Syria umefanikiwa kutungua makombora ya utawala haramu wa Israel viungani mwa mji mkuu wa nchi hiyo ya Kiarabu, Damascus.
Shirika rasmi la habari la Syria SANA limeripoti kuwa, ndege za kijeshi za Israel zimeondosha makombora hayo kutoka Miinuko ya Golan ya Syria inayokaliwa kwa mabavu na mji wa Marj al-Eyoun nchini Lebanon usiku wa kuamkia leo.
Makamanda wa jeshi la Syria wamenukuliwa wakisema mfumo huo wa ngao ya makombora umefanikiwa kutungua aghalabu ya makombora yaliyovurumishwa na jeshi katili la Israel dhidi ya makazi ya raia viungani mwa Damascus.
Duru zingine za habari hata hivyo zimearifu kuwa, makombora mawili ya Wazayuni yaliyolenga majengo ya makazi ya watu yameua watu wawili katika miji ya Saasa na Qudsaya.
Haya yanajiri wakati huu ambapo Marekani inazidi kumimina wanajeshi wake kaskazini mwa Syria, licha ya rais wa Marekani, Donald Trump kudai kuwa ameamua kuondoa wanajeshi wake nchini humo.