Jeshi la Syria latungua ndege isiyo na rubani ya Uturuki
Vyombo vya habari nchini Syria vimetangaza kwamba, jeshi la nchi hiyo limetungua ndege isiyo na rubani ya jeshi la Uturuki katika viunga vya mji wa Qamishli, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
Shirika rasmi la habari la Syria SANA limetangaza kwamba ndege hiyo isiyo na rubani ilitunguliwa katika anga ya kijiji cha 'Hamu' karibu na mji wa Qamishli katika mkoa wa Al-Hasakah, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Kadhalika shirika hilo la habari limelinukuu jeshi la Syria likisema kwamba, askari wa nchi hiyo wamezima shambulio la askari wa Uturuki na makundi ya wabeba silaha wanaoungwa mkono na serikali ya Ankara katika kijiji cha 'Tall Laban' katika viunga vya magharibi mwa eneo la Tall Tamr katika mkoa huo wa Al-Hasakah.
Uvamizi wa jeshi la Uturuki kaskazini mwa Syria uliopewa jina la 'Chemchemi ya Amani' ulianza tarehe 9 Oktoba mwaka huu kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi na kusafisha maeneo ya mpakani ya nchi hiyo jirani ya Kiarabu kutokana na uwepo wa wanamgambo wa Kikurdi ambao serikali ya Ankara inawataja kuwa magaidi. Baada ya kuanza mashambulizi hayo ya Uturuki, Wakurdi waliitaka serikali ya Damascus kudhibiti maeneo ya kaskazini mwa Syria na kuwalinda kutokana na mashambulizi ya Uturuki. Rais Bashar al Assad wa Syria siku chache zilizopita alisisitiza kwamba ikilazimu, jeshi la nchi hiyo litatumia nguvu kuwaondoa askari vamizi wa kigeni waliopo katika ardhi ya nchi hiyo.