Human Rights Watch yakosoa kamatakamata ya wanaharakati nchini Saudia
-
Saudi Arabia
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limetoa taarifa likikosoa hatua ya serikali ya Saudi Arabia ya kuwatia nguvuni maafisa wa serikali, wanaharakati na wakosoaji wa utawala wa nchi hiyo.
Taarifa iliyotolewa na Human Rights Watch imesema kuwa, kutiwa nguvuni watu wasiopungua 298 nchini Saudi Arabia katika siku chache za hivi karibuni kumezidisha wasiwasi kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu nchini humo.
Taarifa hiyo imeitaka serikali ya kifalme ya Saudi Arabia kutangaza haraka tuhuma zinazowakabili mahabusu hao.
Human Rights Watch imesema kuwa suala la kupambana na ufisadi halipasi kufanywa kisingizio cha kuhalalisha ukiukaji wa sheria na haki za binadamu nchini Saudi Arabia.
Jumapili iliyopita vyombo vya habari vya Saudi Arabia viliripoti kuwa, maafisa 298 wa nchi hiyo wakiwemo maafisa kadhaa wa jeshi na polisi wametiwa nguvuni kwa tuhuma za ufisadi na kutumia vibaya madaraka na vyeo vyao.
Mrithi wa ufalme wa Saudia mwanamfalme Muhammad bin Salman pia amemuru kukamatwa mamia ya maafisa wa serikali, wanaharakati wa masuala ya kisiasa, mashekhe na viongozi wa dini na hata wanamfalme kadhaa wa nchi hiyo kwa tuhuma mbalimbali zikiwemo za ufisadi na kupinga utawala wa kifalme wa nchi hiyo.