Baraza la Usalama lataka kusitishwa vita mara moja huko Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i60444-baraza_la_usalama_lataka_kusitishwa_vita_mara_moja_huko_yemen
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeunga mkono pendekezo la Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa la kusitishwa vita mara moja nchini Yemen.
(last modified 2026-08-14T10:24:44+00:00 )
Apr 18, 2020 03:23 UTC
  • Baraza la Usalama lataka kusitishwa vita mara moja huko Yemen

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeunga mkono pendekezo la Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa la kusitishwa vita mara moja nchini Yemen.

José Singer Weisinger, balozi na mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Dominican katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambaye nchi yake ni mwenyekiti wa kiduru wa baraza hilo amewaambia waandishi wa habari kwamba, baraza hilo linaunga mkono pendekezo la Antonio Guterres la kusitishwa vita mara moja huko nchini Yemen.

José Singer Weisinger ameongeza kuwa, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lina wasiwasi na kuendelea vita nchini Yemen hivyo linazitaka pande husika zifanye kila ziwezalo kusitisha vita ili kutoa fursa ya kukabiliana na virusi vya Corona.

Hata hivyo mwenyekiti huyo wa kiduru wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hakuashiria kabisa mashambulio yanayofanywa kila leo na muungano vamizi unaoongozwa na Saudia dhidi ya maeneo mbalimbali ya Yemen ambayo yamezidi kusababisha maafa na uharibifu mkubwa.

José Singer Weisinger, balozi na mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Dominican katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Msemaji wa muungano vamizi huko Yemen unaoongozwa na Saudi Arabia Kanali Turki al Maliki wiki iliyopita alidai kuwa, muungano huo umesitisha vita nchini Yemen.

Hata hivyo katika muda wa wiki moja iliyopita muungano huo vamizi umetekeleza mashambulio ya anga mara 230 na kufanya mashambulizi 32 ya nchi kavu.

Uvamizi wa kikatili wa Saudi Arabia na wavamizi wenzake hasa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) katika nchi maskini ya Yemen umesababisha maafa makubwa ya roho na mali na kuangamiza kila kitu katika nchi hiyo masikini ya Kiarabu.