Ripoti: Mamia ya Wanawafalme Saudia wanaugua corona
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i60452-ripoti_mamia_ya_wanawafalme_saudia_wanaugua_corona
Kuna idadi kubwa ya wanawafalme katika Ufalme wa Saudi Arabia ambao wanaugua ugonjwa wa corona au COVID-19, na idadi yao kamili ni kubwa kuliko ile inayotangazwa na vyombo husika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 18, 2020 07:09 UTC
  • Ripoti: Mamia ya Wanawafalme Saudia wanaugua corona

Kuna idadi kubwa ya wanawafalme katika Ufalme wa Saudi Arabia ambao wanaugua ugonjwa wa corona au COVID-19, na idadi yao kamili ni kubwa kuliko ile inayotangazwa na vyombo husika.

Mvujisha siri wa Saudia ambaye anatumia jina la al-Ahd al-Jadid katika ukurasa wake wa Twitter siku ya Ijumaa alifichua kuwa wanawafalme wa Saudia waliombukizwa corona ni zaidi ya 150 ambao walitangazwa hivi karibuni na gazeti la New York Times.

Gazeti hilo wiki iliyopita liliandika kuwa vitanda 500 vimetengwa katika hospitali ya kifahari ya Mfalme Faisal kwa ajili ya kuwatibu wanawafalme ambao wameambukizwa corona.

Katika  taarifa iliyosambazwa kupitia ukurasa wa Twitter wa al-Ahd al-Jadid, ambalo ni maarufu kwa kuvujisha siri za ndani kabisa za ufalme wa Saudia, imebainika kuwa hospitali hiyo  ya Saudia ambayo imetengwa kwa ajili ya wanawafalme mjini  Jeddah sasa ina msongamano mkubwa kutokana na idadi kubwa ya walioambukizwa corona. ‘Hospitali ya kitaalamu ya Jeddah ambayo imetengwa kwa ajili ya wanawafalme, haiwezi tena kuwapokea wagonjwa,” imesema taarifa hiyo ya Twitter.

Aidha ameongeza kuwa, kutokana na msongamano mkubwa katika hospitali hiyo ya kitaalamu, hoteli mbili zimetengwa kwa ajili ya kuwatibu wanawafalme walioambukizwa corona.

Mohammad bin Salman

Mvujishaji siri mwingine wa Saudia ambaye hutumia akaunti ya Twitter ya ‘Mujtahid’ naye pia ametilia shaka idadi rasmi inayotangazwa kuhusu walioambukizwa corona nchini Saudi Arabia.

Hadi kufikia Aprili 18, idadi ya walioambukizwa COVID-19 nchini Saudi Arabia ilikuwa 7,142 huku waliofariki kutokana na ugonjwa huo wakiwa ni 87.

Imedokezwa kuwa Mfalme Salman wa Saudia, mwenye umri wa miaka 83, ameenda mafichoni katika kasiri iliyo katika mji wa Jeddah katika pwani ya Bahari ya Sham. Aidha Mrithi wa Kiti cha Ufalme, Mwanamfalme Mohammad bin Salman, ambaye kimsingi ndiye mtawala wa sasa wa Saudia, naye pia ameenda mafichoni na mawaziri wake katika eneo kunakojengwa mji mpya unaojulikana kama Neom.