Kuvunjika mazungumzo na kushadidi hitilafu kusini mwa Yemen
Mazungumzo ya serikali iliyojiuzulu ya Abdrabbuh Mansur Hadi na Baraza la Mpito la Kusini mwa Yemen yamevunjika na kutokuwa na natija; na hivyo kwa mara nyingine tena kushadidisha hitilafu baina ya pande mbili hizo.
Hitilafu na mivutano kusini mwa Yemen si jambo jipya. Tunaweza kuzizungumzia hitilafu hizo katika vipindi na awamu tatu tofauti. Awamu ya kwanza ni mwaka 2017. Mwanzoni mwa Aprili mwaka huo, Abdrabbuh Mansur Hadi Rais aliyejiuzulu wa Yemen alimuuzulu Meja Jenerali Aidarus al-Zubaidi kutoka katika cheo chake cha Gavana wa Aden. Muda mfupi baada ya hatua hiyo, yaani mwezi Mei mwaka 2017, Baraza la Mpito la Kusini likatangaza rasmi uwepo wake likiungwa mkono na nchi ya Imarati na kisha likamchagua Aidarus al-Zubaidi kuwa mkuu wa baraza hilo.
Baada ya kuundwa Baraza la Mpito la Kusini mwa Yemen kukaasisiwa Hizam al-Amni (Mkanda wa Usalama) ambalo ni tawi la kijeshi la baraza hilo. Huo ndio uliokuwa mwanzo wa kuibuka hitilafu na mizozo huko kusini mwa Yemen, kwani kivitendo kukawa kumejitokeza nguvu mbili yaani za serikali iliyojiuzulu na Baraza la Mpito.
Awamu ya pili cha hitilafu baina ya pande mbili ni msimu wa joto mwaka 2019. Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) ulitangaza kuwa, unaondoa wanajeshi wake kusini mwa Yemen. Hatua hiyo ilipelekea kuongezeka manuva na harakati za Baraza la Mpito la Kusini sambamba na kushadidi mapigano baina ya baraza hilo na mamluki wa serikali iliyojiuzulu kiasi kwamba, vikosi vya baraza hilo vilifanikiwa kuidhibiti Ikulu ya Rais mjini Aden na makao ya baadhi ya wizara.
Kuendelea mapigano hayo, kulifanya Saudi Arabia ambayo kabla ya hapo haikuwa ikilitambua rasmi Baraza la Mpito, imwalike mjini Riyadh mkuu wa baraza hilo na wajumbe wake kadhaa ili ifanye nao mazungumzo. Hatua hiyo ya Saudia haikuifurahisha serikali iliyojiuzulu ya Mansur Hadi. Natija ya mazungumzo hayo ikawa ni kufikiwa ‘Makubaliano ya Riyadh Novemba 2019’. Kwa mujibu wa makubaliano hayo iliamuliwa kuwa, Baraza la Mpito na serikali iliyojiuzulu ya Mansur Hadi ziweke kando hitilafu zao na kuunda serikali moja na vikosi vya pamoja. Hata hivyo makubaliano hayo yalibakia katika makaratasi tu, kwani hakuna wakati ambao yalitekelezwa kivitendo.
Mivutano na hitilafu za hivi karibuni kusini mwa Yemen ni awamu ya tatu ya mizozo hiyo. Hitilafu za mara hii zilidhihiri na kushadidi baada ya vikosi vyenye mfungamno na serikali iliyojiuzulu ya Mansur Hadi kujiunga na wanamgambo wa Baraza la Mpito la Kusini. Baada ya kushtadi hitilafu hizo, makamanda wa jeshi wa serikali iliyojiuzulu na Baraza la Mpito la Kusini walikutana na kufanya mazungumzo. Hata hivyo mazungumzo hayo nayo yamemalizika bila ya kuwa na tija.
Sababu kuu ya kuvunjika mazungumzo hayo ni kung’ang’ania serikali iliyojiuzulu msimamo wa kuvunjwa vikosi vya Baraza la Mpito na kuunganishwa na vikosi vya Wizara ya Ulinzi ya serikali hiyo, jambo ambalo halikubaliwi na viongozi wa baraza hilo.
Ndio kusema kuwa, kuvunjika mazungumzo hayo maana yake ni kushadidi hitilafu kusini mwa Yemen. Katika uwanja huo, Brigedia Jenerali Abdullah al-Subaihi, kamanda wa Brigedi ya 39 ya mji wa Abyan amewatishia mamluki wenye mfungamano na Imarati kwamba, kama hawatakubaliani na masharti ya serikali iliyojiuzulu ya Yemen basi atatoa amri kwa wanajeshi wake wanaofikia 3,000 kuanzisha vita dhidi ya mamluki hao. Tishio hili ni ithbati tosha kwamba, Baraza la Mpito la Kusini na serikali iliyojuzulu ya Yemen zimo mbioni kuingia vitani.
Filihali, kuvunjika mazungumzo ya Aden ni ujumbe wa wazi wa kusambaratika kikamilifu makubaliano ya Riyadh ya Novemba mwaka jana. Kwani hivi sasa si tu kwamba, hakujaundwa serikali jumuishi na vikosi vya pamoja kusini mwa Yemen kama yalivyokuwa yakitaka makubaliano hayo, bali hata hitilafu za sasa ni kubwa zaidi ikilinganishwa na mizozo iliyokuwako Oktoba na Novemba mwaka uliopita wa 2019.
Nukta ya mwisho ni hii kwamba, kuvunjika mazungumzo ya Aden na kushadidi hitilafu kusini mwa Yemen ni ishara ya wazi kwamba, serikali ya Imarati imo mbioni kubadilisha mlingano katika eneo hilo kwa maslahi ya mamluki wake na kuidhoofisha serikali iliyojiuzulu ya Yemen, ambapo hatua hii nayo inaweza kuwa chimbuko la kushadidi mivutano baina ya tawala za Riyadh na Abu Dhabi.