Balozi wa Syria: Umoja wa Mataifa umefeli kuishinikiza Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i60582-balozi_wa_syria_umoja_wa_mataifa_umefeli_kuishinikiza_israel
Balozi wa Syria katika Umoja wa Mataifa amesema Baraza la Usalama la umoja huo limefeli kuushinikiza utawala wa Kizayuni wa Israel utekeleze maazimio ya baraza hilo kuhusu Palestina na Syria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 24, 2020 23:36 UTC
  • Balozi wa Syria: Umoja wa Mataifa umefeli kuishinikiza Israel

Balozi wa Syria katika Umoja wa Mataifa amesema Baraza la Usalama la umoja huo limefeli kuushinikiza utawala wa Kizayuni wa Israel utekeleze maazimio ya baraza hilo kuhusu Palestina na Syria.

Akizungumza kwa njia ya video katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali katika eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati), Bashar al-Ja'afari, Balozi wa Syria katika Umoja wa Mataifa amesema Baraza la Usalama limeshindwa kuuchukulia hatua utawala ghasibu wa Israel kutokana na mashinikizo ya baadhi ya wanachama wa kudumu wa baraza hilo.

Amesema kati ya maazimio ambayo Umoja wa Mataifa umeshindwa kuyatekeleza ni maazimio nambari 242, 338 na 497 kuhusu ardhi za Waarabu zinazokaliwa kwa mabavu na Israel. Maazimio hayo yanautaka utawala ghasibu  wa Israel uache kukalia kwa mabavu ardhi za Waarabu.

Al- Ja'afari amesisitiza kuwa Miinuko ya Golan inayokaliwa kwa mabavu na Isrel ni sehemu isiyotenganika ya ardhi ya Syria na kuongeza kuwa, kusitishwa ukaliwaji mabavu eneo hilo la kistratijia ni kipaumbele cha serikali ya Syria.

Mji wa Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel

Aidha amesema hatua ya Umoja wa Mataifa ya kutofuatilia utekelezwaji wa maazimio hayo ni jambo ambalo limezichochea nchi zingine duniani kuacha kutekeleza majukumu ya kisheria na kubadilisha ukweli wa mambo. Amebaini kuwa mfano wa nukta hiyo ni ile hatua ya kichokozi ya Marekani ya kutambua mji wa Quds (Jerusalem) kuwa mji mkuu wa utawala haramu wa Israel mwezi Disemba 2017 na baada ya hapo kutambua  rasmi 'umiliki' wa Israel wa Miinuko ya Golan mnamo Machi 2019.