Saudia yakumbwa na mgogoro mkubwa wa kiuchumi, mishahara yapunguzwa
Janga la COVID-19 limeshadidisha mgogoro wa kiuchumi Saudia Arabia na sasa mishahara ya wafanyakazi katika sekta binfasi nchini humo imepunguzwa kwa asilimia 40.
Leo Jumatano, utawala wa Saudia umetoa taarifa na kusema mikataba itaangaliwa upya ambapo mashirika binafsi na ya serikali yanaweza kubadilisha miktaba wakati wowote ule.
Gazeti la Asharq al-Awsat pia nalo limechapisha mikataba mipya ya wafanya kazi wa Saudia ambapo wakandarasi wanaruhusiwa kupunguza mishahara kwa asilimia 40 katika kipindi cha miezi sita na baada ya hapo wanaweza kubatilisha mikataba hiyo.
Saudi Arabia ni kati ya nchi zinazouza mafuta kwa wingi duniani lakini kutokana na sera za ubabe za Mohammad bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme, nchi hiyo ilianzisha vita dhidi ya Yemen na imekuwa ikizozana na Russia kuhusu bei ya mafuta mambo ambayo yameitumbukiza katika mgogoro mkubwa wa kifedha na kiuchumi.
Ripoti zinaonyesha kuwa umasikini umekithiri sana miongoni mwa wananchi wa Saudia huku raia wa kigeni wanaofanya kazi nchini humo wakikumbwa na masaibu kutokana na mazingira mabaya ya kikazi.
Kwa mujibu wa takwimu rasmi, kuhusu ugojwa wa COVID-19, hadi sasa watu 30,351 wameambukizwa ugonjwa huo nchini humo huku waliofariki wakiwa ni 200.