Rais Rouhani aitahadharisha Marekani kuhusu kutatiza meli za mafuta za Iran
(last modified Sun, 24 May 2020 07:49:54 GMT )
May 24, 2020 07:49 UTC
  • Rais Rouhani aitahadharisha Marekani kuhusu kutatiza meli za mafuta za Iran

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria baadhi ya chokochoko za Marekani katika eneo la Bahari ya Caribbean na kusema: "Iwapo meli za mafuta za Iran zitakabliwa na tatizo lolote kutoka Marekani, basi Iran nayo itawaibulia matatizo."

Rais Hassan Rouhani aliyasema hayo Jumamosi katika mazungumzo ya simu na Emir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad al-Thani na kuongeza kuwa, usalama wa eneo ni muhimu sana kwa Iran. Rais Rouhani ameongeza kuwa: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina haki ya kisheria ya kulinda mamlaka yake ya kujitawala na hivyo Tehran inatumai kuwa Marekani haitafanya kosa."

Tayari meli ya kwanza ya mafuta ya Iran imeshawasili katika maji ya Venezuela ikiwa na shehena ya mafuta ya petroli. Kwa ujumla Iran imetuma meli tano za petroli nchini Venezeual. Pamoja na kuwa Venezuela ina utajiri mkubwa wa mafuta ghafi ya petroli lakini viwanda vyake vya kusafisha mafuta havifanyi kazi kutokana na vikwazo vya Marekani. Viongozi wa Marekani wanadai kwamba mauzo ya mafuta ya Iran kwa Venezuela ni kinyume cha sheria na kwamba ni lazima wakabiliane na suala hilo. Ni kwa msingi huo ndipo wakatuma askari wa baharini wa Marekani karibu na maji ya Venezuela.

Kwingineko katika mazungumzo yake na Emir wa Qatar, Rais Rouhani amesisitiza kuwa, usalama wa eneo la Asia Magharibi hasa usalama wa baharini unapaswa kudhaminiwa na nchi za eneo na amekumbusha kuwa, Iran iko tayari kushirikiana na nchi jirani katika uga huo.

Meli ya mafuta

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amsema uhusiano wa Iran na Qatar ni wa kirafiki na kistratijia na ameelezea matumaini yake kuwa: "Pamoja na kuwepo janga la COVID-19, usafirishaji bidhaa baina ya bandari za Iran na Qatar utaanza taratibu na kushika kasi na vilevile safari za ndege baina ya nchi mbili."

Kwa upande wake, Emir wa Qatar amesisitiza kuhusu kuimarishwa uhusiano wa Iran na Qatar katika nyanja zote na ameeleza matumaini kuwa katika kikao cha pamoja  cha kiuchumi baina ya nchi mbili, uhusiano wa kibiashara na kiuchumi wa Iran na Qatar utaimarishwa.

Sheikh Tamim bin Hamad al-Thani aidha amesisitiza kuwa, usalama wa eneo unapaswa kudhaminiwa kwa ushirikiano wa nchi za eneo na kuongeza kuwa, Qatar inapinga taharuki yoyote katika eneo.

Tags