Kamisheni ya UNESCO ya Yemen yataka Saudia ishtakiwe ICC
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i61781-kamisheni_ya_unesco_ya_yemen_yataka_saudia_ishtakiwe_icc
Kamisheni ya Kitaifa ya Yemen katika Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) imeutaka Umoja wa Mataifa uangalie upya uamuzi wake wa kufuta jina la Saudi Arabia na washirika wake katika vita vya Yemen kwenye orodha nyeusi ya nchi zinazoua watoto na kuvunja haki zao, na badala yake uwasilishe faili la jinai hizo katika Mahakama ya Kimataifa ya Jina (ICC).
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 23, 2020 23:18 UTC
  • Kamisheni ya UNESCO ya Yemen yataka Saudia ishtakiwe ICC

Kamisheni ya Kitaifa ya Yemen katika Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) imeutaka Umoja wa Mataifa uangalie upya uamuzi wake wa kufuta jina la Saudi Arabia na washirika wake katika vita vya Yemen kwenye orodha nyeusi ya nchi zinazoua watoto na kuvunja haki zao, na badala yake uwasilishe faili la jinai hizo katika Mahakama ya Kimataifa ya Jina (ICC).

Taarifa iliyotolewa jana Jumanne na kamisheni hiyo ya kitaifa ya Yemen imesema uamuzi huo wa UN umepuuza ushahidi uliotolewa na baadhi ya wanachama wenyewe wa muungano vamizi wa kijeshi wa Saudia katika vita dhidi ya Yemen, waliokiri kuwa muungano huo umehusika katika kuwaua, kuwaacha njaa kwa makusudi na kuwapa vichapo vikali watoto wa Yemen.

Kamisheni ya Kitaifa ya Yemen katika shirika la UNESCO imesema, kitendo cha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres cha kutangaza kuwa muungano wa vita vya Yemen unaoongozwa na Saudi Arabia umeondolewa katika 'orodha ya fedheha' ya taasisi hiyo ya wauaji na wavunjaji wakubwa wa haki za watoto, hakitakuwa na matokeo mengine ghairi ya kuufungulia mlango muungano huo kutenda jinai zaidi na kukanyaga sheria za kimataifa.

Kamisheni hiyo imeeleza bayana kuwa, anachotakiwa kufanya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ni kuwasilisha faili la jinai za muungano huo wa kijeshi wa Riyadh katika Mahakama ya Kimataifa ya Jina (ICC) iliyoko mjini The Hague nchini Uholanzi.

 

Jinai za kutisha dhidi ya watoto wa Yemen

Mashirika mbali mbali ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu kama vile Amnesty International, Human Rights Watch na Save the Children yamemjia juu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na kukosoa vikali uamuzi wake huo, yakisisitiza kuwa, kwa kutoubebesha dhima muungano huo vamizi wa Saudia na Imarati, Katibu Mkuu wa UN amewaweka watoto wa Yemen katika hatari zaidi ya kuendelea kushambuliwa. 

Mwaka 2017 Umoja wa Mataifa uliiweka Saudi Arabia katika orodha nyeusi ya wauaji na wakiukaji wakubwa wa haki za watoto kutokana na mauaji ya maelfu ya watoto wa Yemen na kuharibiwa shule na mahospitali ya nchi hiyo katika mashambulizi ya Saudia.