Maandamano mtawalia dhidi ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu
Ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) kwa mara ya kadhaa zimeshuhudia maandamano mtawalia ya wananchi katika kipindi cha miezi miwili ya hivi karibuni dhidi ya Baraza la Mawaziri la Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.
Katika maandamano ya juzi Julai 11, dhidi ya serikali ya Netanyahu, takribani watu 10,000 walijitokeza mjini Tel-Aviv na kushiriki maandamano hayo. Mei 17 mwaka huu, Netanyahu alifanikiwa kuunda serikali mpya baada ya kufanyika chaguzi tatu za Bunge. Kwa sasa serikali yake inakabiliwa na changamoto muhimu ya kutokuweko mshikamano wa ndani na kukosekana hali ya kuaminiana baina ya mawaziri hususan kutoaminiwa Netanyahu. Hiyo inatokana na kuwa, baraza hilo la mawaziri limeundwa kwa lazima na kutokana na mazingira yaliyokuwako baada ya kuibuka mkwamo wa kisiasa. Kulazimika kuunda baraza hilo la mawaziri kulitokana na kushindwa chama cha Likud kupata viti mutlaki ambavyo ni asilimia 50+1. Hii ni katika hali ambayo, kufanyika duru tatu za uchaguzi wa Bunge kumeutwisha utawala huo ghasibu mzigo mkubwa wa gharama na mwishowe Netanyahu na Benny Ganzt wakafikia makubaliano ya kuunda serikali jumuishi.
Licha ya kuwa makubaliano hayo yamehitimisha kwa muda mkwamo wa kisiasa huko Israel, lakini baraza jipya la mawaziri la Israel linakabiliwa na changamoto nyingine muhimu ambapo kusambaa virusi vya corona sambamba na matatizo ya kiuchumi ni miogoni mwa changamoto muhimu zaidi ambazo zimeandaa uwanja wa kufanyika maandamano dhidi ya serikali ya Benjamin Netanyahu.
Kushindwa serikali ya Netanyahu kukabiliana na virusi vya corona ni moja ya sababu za kufanyika maandamano. Kwa mujibu wa mtandao wa worldometers hadi sasa zaidi ya watu 38,000 wameambukizwa virusi vya corona katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) na karibu 400 wameaga dunia. Pamoja na hayo wakosoaji wa Netanyahu wanaamini kwamba, idadi ya maambukizo na vifo vya corona vinavyotangazwa haikisi uhalisia kwani ni zaidi ya hiyo.
Hali mbaya ya uchumi ni sababu nyingine ya kushuhudiwa wimbi la maandamano huko Israel. Baadhi ya takwimu na uchunguzi wa maoni uliofanywa na vituo vya Israel unaonyesha kuwa, ukosefu wa ajira unaongeza kiasi kwamba, kiwango cha ukosefu wa ajira kimefikia asilimia 26. Hapo kabla pia, Wizara ya Uchumi ya utawala haramu wa Israel ilikuwa imetangaza katika ripoti yake kwamba, kuanzia mwezi Machi mpaka Mei mwaka huu, kulisajiliwa maombi milioni 1.5 ya kupokea upendeleo wa kukosa ajira. Kadhalika asilimia 21 ya wakazi wa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu walipoteza nyumba zao katika kipindi cha miezi minne ya kusambaa virusi vya corona na kulazimika kurejea katika nyumba za wazazi wao.
Ufisadi wa kifedha ni sehemu nyingine iliyochangia kuibuka maandamano ya wananchi huko Israel. Netanyahu anakabiliwa na mafaili manne ya ufisadi. Hata hivyo akitumia lobi na mashinikizo aNetanyahu meweza kusogeza mbele tarehe ya kusikilizwa kesi zake na kuunda serikali na hatimaye kukwepa tuhuma hizo kwa kutumia kinga ya kisiasa.
Pamoja na hayo, suala hilo halijawafanya wakazi wa Israel wasahau mafaili ya ufisadi ya Netanyahu. Katika fremu hiyo na katika maandamano ya Jumamosi iliyopita, waandamanaji waikuwa wamebeba mabango na maberamu ambapo baadhi ya jumbe zake zilisomeka: “Rushwa, utapeli na usaliti katika amani”. Aidha waandamanaji hao walikuwa wakipiga nara za kutaka kupambana na ufisadi wa kifedha wa Netanyahu.
Jambo muhimu ni hili kwamba, Netanyahu na baraza lake la mawaziri badala ya kutanguliza mbele matatizo ya kiafya na kiuchumi yanayoisumbua Israel kwa sasa, wameng’ang’ania kusukuma mbele gurudumu la mipango ya kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina ukiwemo mpango wa kutwaa asilimia 30 ya eneo la Palestina la Ukingo wa Magharibi na kuliunganisha na ardhi nyingine zilizoghusubiwa za Palestina. Wakati huo huo, baadhi ya duru za Israel zimeripoti kuwa, chama cha Blu na Nyeupe cha Benny Gantz ambacho kinahesabiwa kuwa muitifaki wa Netanyahu katika kuunda serikali na ambaye ni Waziri wa Vita kimeatangaza kuunga mkono maandamano hayo yaliyo dhidi ya Netanyahu, msimamo ambao unaonesha ni kwa jinsi gani serikali ya Waziri Mkuu wa Israel inakabiliwa na mgawanyiko.