Zarif: Iran daima inataka uhusiano mwema baina ya Baghdad na Arbil
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i62308-zarif_iran_daima_inataka_uhusiano_mwema_baina_ya_baghdad_na_arbil
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema daima Tehran imekuwa ikitaka kuwepo uhusiano mwema baina ya Baghdad na Arbil.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 20, 2020 02:30 UTC
  • Zarif: Iran daima inataka uhusiano mwema baina ya Baghdad na Arbil

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema daima Tehran imekuwa ikitaka kuwepo uhusiano mwema baina ya Baghdad na Arbil.

Mohammad Javad Zarif Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aliyasema hayo Jumapili usiku wakati akiwa mjini Arbil alipokutana na kufanya mazungumzo na Masoud Barzani, Rais wa Eneo la Kurdistan lenye mamlaka ya ndani nchini Iraq. Katika mkutano huo, Zarif amesisitiza kuhusu umuhimu wa mamlaka ya kujitawala Iraq sambamba na kuimarishwa uhusiano wa pande zote baina ya Iraq na Iran.

Kwa upande wake Masoud Barzani ameashiria mshikamano imara wa mataifa mawili ya Iran na Iraq pamoja na nafasi isiyosahaulika ya Shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani katika kulisambaratisha kundi la kigaidi la ISIS (Daesh) na kusisitiza kuwa: "Eneo la Kurdistan la Iraq  katu halitakuwa tishio kwa maslahi na usalama wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Rais wa Eneo la Kurdistan ambaye pia ni mwenyekiti wa Chama cha Kidemokrasia cha Kurdistan ya Iraq aidha wamesisitiza kuhusu kuimarishwa mabdilishano ya kibiasahra kwa kuzigatiwa kanuni na protokali za Kiafya.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran jana Jumapili aliwasili katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad, kwa lengo la kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi hiyo na alasiri ya jana akaelekea Arbil, mji mkuu Eneo la Kurdistan.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif (kushoto) na Waziri Mkuu  wa Iraq Mustafa Al Kadhimi

Akiwa Baghdad Zarif alikutana na Rais wa Iraq Barham Salih, Waziri Mkuu Mustafa Al Kadhimi, Waziri wa Mambo ya Nje Hadi Al Amiri, Mwenyekiti wa Muungano wa Al Fath Sayyid Ammar Hakim pamoja na viongozi wengine wa nchini humo. Punde baada ya kuwasili mjini Baghdad, Zarif alitembelea eneo ambalo waliuawa shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani na Abu Mahdi al Muhandis pamoja na walioandamana nao karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad. 

Itakumbukwa kuwa shahidi Qassem Soleimani, na Abu Mahdi al-Muhandis Naibu Kamanda wa Kikosi cha kujitolea cha wananchi wa Iraq, Al Hashd Al Shaabi, waliuawa wakiwa na wenzao wengine wanane tarehe tatu Januari mwaka huu, katika shambulio la kigaidi lililotekelezwa na askari magaidi wa Marekani karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa wa mjini Baghdad, Iraq. Shahidi Soleimani alikuwa nchini Iraq kufuatia mwaliko rasmi wa wakuu wa nchi hiyo.