Uasi dhidi ya Netanyahu
Kwa wiki ya nne mfululizo, wapinzani katika utawala ghasibu wa Israel, wameandama mbele ya nyumba ya Benjamini Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala huo kupinga siasa zake mbovu na ufisadi wa mwanasiasa huyo.
Netanyahu amekuwa akikabiliwa na matatizo mengi katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu uliopita, moja ya matatizo hayo ikiwa ni kushindwa kwake kubuni kwa wakati baraza la mawaziri. Jambo hilo limemlazimu kugawana madaraka na hasimu wake mkuu wa kisiasa Benny Gantz wa chama cha Buluu na Nyeupe ili aendelee kubakia madarakani.
Pamoja na hayo juhudi zake hizo zimetumbukia hatarini tena. Faili na ufisadi la waziri mkuu huyo limefunguliwa katika hali ambayo raia wa utawala wa Israel wanapitia kipindi kigumu cha ughali wa maisha. Katika miaka kadhaa iliyopita Netanyahu amekabiliwa na mafaili manne ya ufisadi na ubadhirifu wa fedha. Faili la kwanza ambalo linajulikana kama Faili la 1000 linahusiana na kupokea kwake hongo na zawadi za kutiliwa shaka kutoka kwa wafanyabiashara tajiri. La pili ambalo linajulikana kama Faili la 2000 pia linahusiana na mapatano yake na mmiliki wa gazeti la Kizayuni la Yedioth Ahronoth kwa ajili ya kutangaza na kuakisi vizuri habari zinazohusiana na baraza lake la mawaziri mkabala na kuwekewa vikwazo mshindani mkuu wa gazeti hilo, yaani gazeti la Israel Hayom.
Faili la tatu ambalo ni mashuhuri kwa jina la Faili la 3000 linahusiana na waziri mkuu huyo kupokea hongo kwa ajili ya kufanikisha manunuzi ya nyambizi za atomiki kutoka Ujerumani. Katika faili la nne pia ambalo ni mashuhuri kwa jina la Faili la 4000 Netanyahu anatuhumiwa kumlipa kinyume cha sheria Shaul Elovitch, mfanyabiashara mashuhuri wa Kizayuni, mamilioni ya dola.
Mwishoni mwa mwezi Februari mwaka huu, mwendesha mashtaka wa utawala haramu wa Israel alimtuhumu Netanyahu katika mafaili matatu ya 1000, 2000 na 4000 kwa ulaji rushwa, ulaghai na kutolinda amana. Netanyahu ametumia vibaya ushawishi wake katika vyombo vya mahakama vya Israel kutaka kufunika mafaili hayo, lakini Wazayuni ambao kwa sasa wanapitia hali ngumu ya maisha katika mazingira haya ya kuenea virusi vya corona, wamemiminika mitaani wakimtaka waziri mkuu huyo ajiuzulu mara moja.
Avigdor Lieberman, waziri wa zamani wa vita wa utawala wa Kizayuni amesema kuwa kwa kuzingatia hali ambaya ya uchumi wa utawala huo, kuna uwezekano mkubwa wa utawala huo kushuhudia karibuni uasi wa raia. Gazeti la Yedioth Ahronoth pia limechapisha makala inayokosoa utendaji wa serikali ya Netanyahu katika kukabiliana na mgogoro wa virusi vya corona na kusema kuwa waziri mkuu huyo ni hatari kubwa kwa Wazayuni kuliko hata virusi hivyo. Linasema katika hali ambayo Wazayuni wanakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kiuchumi Netanyahu anaendelea kutumia fedha nyingi za umma kwa lengo la kujitetea dhidi ya mafaili ya ufisadi wa kifedha.
Ili kukabiliana na mashinikizo ya raia wa utawala huo haramu, Netanyahu ametoa pendekezo la kuzipa familia zilizo na watu watatu dola 583, watu wanne dola 729 na watu watano na zaidi dola 875. Watu ambao hawajaoa au kuolewa watapewa dola 218.
Nukta ya kuzingatiwa hapa ni kuwa pendekezo hilo halijakubaliwa hata ndani ya serikali ya Netanyahu mwenyewe. Chama cha Buluu na Nyeupe cha Benny Gantz ambaye kwa sasa ni Waziri wa Vita wa Israel kimekosoa mbinu hiyo ya familia kupewa pesa tasilimu na badala yake kinata familia masikini tu na zisizo na uwezo mkubwa wa kifedha kupewa fedha hizo.
Kuenea kwa kasi virusi vya corona katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) bila shaka kutazidisha matatizo ya kimaisha ya Wazayuni na hivyo kuwachochea wadumishe maandamano na malalamiko dhidi ya Netanyahu mfisadi.