Nyakati "ngumu zaidi" kwa Benjamin Netanyahu katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i62521-nyakati_ngumu_zaidi_kwa_benjamin_netanyahu_katika_ardhi_zinazokaliwa_kwa_mabavu
Maandamamano ya kumshinikiza Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala ghasibu wa Israel ajiuzulu yanaongezeka na kushadidi kila siku. Netanyahu amekuwa Waziri Mkuu wa Israel tangu mwaka 2009.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 31, 2020 02:31 UTC
  • Nyakati

Maandamamano ya kumshinikiza Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala ghasibu wa Israel ajiuzulu yanaongezeka na kushadidi kila siku. Netanyahu amekuwa Waziri Mkuu wa Israel tangu mwaka 2009.

Akipata himaya na uungaji mkono wa kila upande wa serikali ya Marekani, hadi kufikia mwaka jana 2019 mwanasiasa huyo mambo yalikuwa yakimwendea vizuri kabisa na uongozi wake haukukabiliwa na tishio, kwani hakukuwa na mshindani wa kutisha wa cheo cha Waziri Mkuu na ndio maana alikuwa akiunda kirahisi Baraza la Mawaziri.

Hata hivyo kuanzia mwaka jana upepo uligeuka huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu na mambo yakaanza kwenda kinyume na matarajio ya Netanyahu. Katika mwezi mmoja wa hivi karibuni, mambo yamemuendea mrama zaidi Netanyahu na kutishia uhai wa maisha yake ya kisiasa ambapo uwezekano wa kuanguka kisiasa umepata nguvu zaidi.

Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala ghasibu wa Israel

Hata kama Netanyahu anaona malalamiko na mashinikizo ya Waisraili chimbuko lake ni kuenea virusi vya corona, lakini wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, virusi vya corona vimechochea tu malalamiko na kuwafanya wapinzani wake wapate nguvu zaidi ya kupigia upatu takwa lao la kujiuzulu Waziri Mkuu huyo wa Israel.

Matatizo ya kiuchumi huko Israel yameshadidi kutokana na kushindwa Baraza la Mawaziri la Netanyahu kukabiliana na virusi vya corona. Hata hivyo matatizo hayo yamekuweko katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita ambapo Israel imekuwa ikikabiliwa na mgogoro wa kisiasa. Netanyahu amekuwa akikabiliwa pia na mafaili manne makubwa ya ufisadi.

Ukweli wa mambo ni kuwa, kile ambacho kimemporomosha kisiasa Netanyahu huko Israel ni hatua yake ya kutanguliza maslahi binafsi mbele ya maslahi ya umma sambamba na kupuuza kabisa matarajio ya wananchi. Waandamanaji wakiwa wamebeba mabango yenye maandishi Last Supper "Mlo wa Mwisho wa Jioni" wamesema kuwa, maisha ya kisiasa ya Netanyahu yamefikia tamati.

Mgomo wa wauguzi Israel wakilalamikia uzembe wa serikali ya Netanyahu katika kushughulia uhaba wa suhula za tiba hasa katika kipindi hiki cha maambukizo ya corona

Netanyahu mbali na kupoteza uungaji mkono wa wananchi, hivi sasa anashuhudia pia kuongezeka malalamiko katika muundo wa chama chake cha Likud. Hii ni kutokana na kuwa, nafasi ya chama cha Likud nayo imeporomoka kutokana na utendaji mbovu wa Netanyahu.

Matokeo ya uchunguzi mpya wa maoni huko Israel (Palestina inayokaliwa kwa mabavu) yanaonyesha kuwa, uungaji mkono wa wananchi kwa chama cha Likud kinachoongozwa na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu unaendelea kupungua kwa kasi siku baada ya siku. Uchunguzi wa maoni uliotangazwa na Radio ya Israel unaonyesha kuwa, katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, chama cha Likud kimepoteza viti 10 na hivyo kuzidi kuporomoka.

Kwa kuzingatia hali hii, inaonekana kuwa Netanyahi anakabiliwa na wakati mgumu kwa sasa na hata mgumu zaidi katika sikuu za usoni, kwani mbali na wananchi, ndani ya chama wa Likud pia kuna makada waandamizi wanaotaka kumuondoa katika cheo cha kiongozi wa chama na hatimaye kumuondoa katika nafasi ya Waziri Mkuu.

Roboti ya Netanyahu iliyotengenezwa na waandamanaji wakimuonyesha akila chakla chake cha mwisho cha jioni (Last Supper) kama ishara ya kufikia tamati maisha yake ya kisiasa.

Baadhi ya ripoti zimefichua kuwa, viongozi wa zamani na wa sasa wa Chama cha Likud kinachoongozwa na Netanyahu wamo mbioni kufikia makubaliano ya kumuondoa Netanyahu kama kiongozi mkuu wa chama na kumuweka mtu mwingine mahala pake. Viongozi waandamizi wa Likud wanasema kuwa, Netanyahu amekengeuka malengo ya chama na hata ya muungano wa mrengo wa kulia na amekuwa akijihusisha na masuala yake binafsi kama vile kushughulikia mafaili ya ufisadi yanayomkabili.

Nukta muhimu na ya kuzingatia ni radiamali ya Netanyahu kuhusu kuongezeka malalamiko dhidi yake. Waungaji mkono wa Waziri Mkuu huyo wamewashambulia waandamanaji na kuwajeruhi. Radiamali hiyo imemfanya Yair Lapid mkuu wa chama cha Yesh Atid na kiongozi wa upinzani katika Bunge la Israel aibuke na kusema kuwa, mikono ya Netanyahu imetakaa damu na kumbebebesha Netanyahu mzigo wa vitendo vya utumiaji mabavu na umwagaji damu huko Tel Aviv. Yair ameonya kwamba, utendaji huu wa Netanyahu utaitumbukiza Israel katika vita ndani.