Ndege za kivita za Saudia zaua watoto katika hujuma Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i62669-ndege_za_kivita_za_saudia_zaua_watoto_katika_hujuma_yemen
Utawala wa Saudia umetekeleza jinai nyingine Yemen katika hujuma mpya ambayo imepelekea raia wasiopungua 21, wakiwemo watoto, kuuawa au kujeruhiwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 07, 2020 06:04 UTC
  • Ndege za kivita za Saudia zaua watoto katika hujuma Yemen

Utawala wa Saudia umetekeleza jinai nyingine Yemen katika hujuma mpya ambayo imepelekea raia wasiopungua 21, wakiwemo watoto, kuuawa au kujeruhiwa.

Kwa mujibu wa Televisheni ya Al Masirah, ndege za kivita za Saudia zimedondosha mabomu katika makazi ya raia huko Al Jawf kaskazini mwa Yemen.

Wizara ya Afya ya Yemen imesema katika hujuma hiyo watu 9 waliuawa, wengi wakiwa ni watoto na wanawake huku wengine 12 wakijeruhiwa vibaya.

Mwezi Julai pia, ndege za kivita za Saudia zililenga sherehe ya harusi katika mji wa Al-Hazm katika mkoa wa al-Jawf na kuua watu 35.

Inafaa kuashiria kuwa, Saudia ilianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mwishoni mwa mwezi Machi 2015 kwa lengo la kuiondoa madarakani Harakati ya Ansarullah na kumrejesha usukani Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kukimbilia Riyadh. 

Ndege ya kivita ya Saudia

Hivi karibuni kituo cha Haki za Binadamu cha Ainul Insaniya kimetoa ripoti na kutangaza kuwa, tokea muungano wa Saudia uanzishe vita dhidi ya Yemen mnamo Machi 26, 2015 hadi sasa, watu 16, 672 wamepoteza maisha moja kwa moja kutokana na vita hivyo na miongoni mwao kuna watoto 3,742 na wanawake 2,364.

Idadi kubwa ya watoto na wanawake ni miongoni mwa waliopoteza maisha moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja kutokana na vita dhidi ya Yemen vinavyoongozwa na Saudia kwa himaya ya madola ya Magharibi hasa Marekani na utawala haramu wa Israel.