Maelfu wakusanyika mbele ya makazi ya Benjamin Netanyahu wakitaka ajiuzulu
Maelfu ya waandamanaji wenye hasira wamekusanyika mbele ya makazi ya Waziri Mkuu wa utawala ghasibu wa Israel Benjamin Netanyahu yaliyopo katika mtaa wa Balfour huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel) na kutaka mwanasiasa huyo ajiuzulu.
Duru za habari zinaripoti kutoka Tel-Aviv kwamba, waandamanaji wapatao 10,000 usiku wa kuamkia leo walikusanyika mbele ya makazi ya Netanyahu wakiwa wamebeba mabango na maberamu na kupiga nara za kujiuzulu Waziri Mkuu huyo wa Israel.
Waandamanaji hao wamekuwa wakisisitiza kuwa, Netanyahu anapaswa kujiuzulu wadhifa wa Waziri Mkuu na kuachana kabisa na siasa kwani anakabiliwa na tuhuma nyingi za ufisadi na kwamba, serikali yake imeshindwa kukabiliana na janga la virusi vya Corona.
Katika miezi ya karibuni Netanyahu amekabiliwa na kesi nne za ufisadi wa fedha; mafaili ambayo yametajwa na vyombo vya habari kwa majina ya faili la 1000, faili la 2000, faili la 3000 na faili la 4000.

Netanyahu na baraza lake la mawaziri wanalaumiwa na waandamanaji hao wanaosema kuwa, badala ya kutanguliza mbele matatizo ya kiafya na kiuchumi yanayoisumbua Israel kwa sasa, wameng’ang’ania kusukuma mbele gurudumu la mipango ya kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina.
Hivi karibuni baadhi ya duru za Israel ziliripoti kuwa, chama cha Blu na Nyeupe cha Benny Gantz ambacho kinahesabiwa kuwa muitifaki wa Netanyahu katika serikali na ambaye ni Waziri wa Vita kimekuwa kikiunga mkono maandamano hayo yaliyo dhidi ya Netanyahu, msimamo ambao unaonesha ni kwa jinsi gani serikali ya Waziri Mkuu wa Israel inakabiliwa na mgawanyiko.