China yaitaka jamii ya kimataifa ishughulikie mgogoro wa Palestina
-
Zhang Jun
Mwakilishi wa China katika Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kupatikana suluhisho la mgogoro wa Palestina.
Zhang Jun amesema katika mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa uliofanyika jana kwa njia ya video kwamba, suala la kuharibiwa muundo wa Palestina katika eneo la Ukingo wa Magharibi linalowalazimisha Wapalestina zaidi kuwa wakimbizi, linatia wasiwasi.
Zhang Jun amesema kuwa, zinapaswa kufanyika jitihada za kutekeleza azimio nambari 2334 la Baraza la Usalama la UN linalohimiza kusitishwa shughuli zote za ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi ya Palestina, kuharibiwa makazi na mashamba ya raia na kusitishwa ukatili na mashambulizi dhidi ya Wapalestina.
Mwakilishi wa China katika Umoja wa Mataifa pia ametoa wito wa kuondolewa mzingiro wa muda mrefu wa Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Ghaza na kusema: Suala hilo litaruhusu kupelekwa misaada ya kibinadamu na huduma nyingine kwa wakazi wa eneo hilo.
Utawala haramu wa Israel unaendeleza ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi iliyoghusubiwa ya Palestina licha ya upinzani wa jamii ya kimataifa na kinyume na maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.