Uturuki yaionya Imarati, yasema inacheza na moto, itakiona cha mtema kuni
Mivutano baina ya Uturuki na Imarati sasa imetoka katika malumbano na vita vya maneno na vyombo vya habari kuhusiana na kadhia ya Libya na kuelekea kwenye mapigano ya kijeshi katika eneo la Bahari ya Mediterania.
Afisa mmoja wa serikali ya Uturuki ambaye jina lake halikutajwa amesema kuwa Imarati inajivika joho lisilokuwa saizi yake na kucheza na moto na kwamba: Iwapo ndege za kivita za Imarati zitakaribia mipaka ya majini ya Uturuki zikatabiliwa na jibu kali.
Uturuki imetoa vitisho hivyo baada ya kutangazwa kwamba, Imarati, Ugiriki na waitifaki wake zitafanya mazoezi ya kijeshi katika Bahari ya Mediterania. Viongozi wa Ugiriki wanaamini kuwa mazoezi ya pamoja ya kijeshi na Imarati na waitifaki wengine wa nchi hiyo katika Bahari ya Mediterania ni hatua ya kujilinda dhidi ya harakati za Uturuki. Kabla ya hapo Uturuki pia ilikuwa imefanya mazoezi kama hayo katika Bahari ya Mediterania.
Mbali na mizozo na mivutano ya Uturuki na Ugiriki ambayo ina sababu za kihistoria, hapana shaka kuwa, matatizo ya Uturuki na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) yana asili na mizizi katika baadhi ya malengo ya kisiasa, kidini na kimadhehebu ya nchi hizo mbili. Nchi mbili za Uturuki na Imarati zimekuwa zikivutana na kulumbana kuhusiana na masuala ya kikanda katika miaka kadhaa ya hivi karibuni. Faili la Syria, uungaji mkono wa Uturuki kwa Qatar mkabala wa vikwazo vya baadhi ya nchi za Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi (GCC), kadhia ya Ikhwanul Muslimin, jaribio la mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Rais Recep Tayyip Erdoğan mwezi Julai mwaka 2016, mapinduzi ya jeshi la Misri dhidi ya serikali ya Mohammed Morsi na sasa mgogoro wa Libya, yote hayo yamezusha mzozo mkubwa baina ya pande hizo mbili na kuzidisha hitilafu baina ya Ankara na Abu Dhabi. Hitilafu hizo zimeshadidi zaidi katika siku za hivi karibuni hususan kuhusu kadhia ya Libya. Imarati inaituhumu Uturuki kwamba inaingilia mambo ya ndani ya nchi hiyo ya Afrika na kwamba inaunga mkono ugaidi. Abu Dhabi pia imeliandikia barua Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ikiituhumu Ankara kuwa inafanya mikakati ya kuzusha ghasia katika nchi za Kiarabu na kutangaza kuwa: Operesheni za kijeshi za Uturuki nchini Syria zinakiuka sheria za kimataifa.
Hapana shaka yoyote kwamba, viongozi wa serikali ya Uturuki hawawezi kustahamili utunishaji misuli wa kijeshi wa nchi kama Imarati na wanasisitiza kuwa ni jambo lisilokubalika kwa Abu Dhabi kujiunga na wapinzani wa Ankara.
Katika miaka ya karibuni nchi ya Imarati ambayo kwa miaka mingi imekuwa imetengwa na kuwekwa kando katika masuala ya siasa za kimataifa, imevimbisha kichwa na kutaka kutunisha misuli ya kijeshi kwa nchi za magharibi mwa Asia hususan Uturuki. Profesa Mehmaet Prinjek, mchambuzi wa masuala ya kisiasa, mjumbe wa Kamati ya Sayansi ya Chuo Kikuu cha Moscow ambaye pia ni mkuu wa Taasisi ya Utafiti ya Chuo Kikuu cha Istanbul anaamini kuwa: Israel, Marekani, Cyprus na Ugiriki zimeanzisha muungano dhidi ya Uturuki huko mashariki mwa Bahari ya Mediterania. Nchi na tawala hizo zinafanya harakati dhidi ya usalama wa Uturuki ambayo ina maslahi muhimu katika kadhia ya Cyprus, Libya na mashariki mwa Mediterania. Serikali ya Imarati pia inatekeleza siasa zinazokinzana na maslahi ya Uturuki huko mashariki mwa Bahari ya Mediterania.
Kwa sasa nchi mbili za Imarati na Uturuki zimesimama katika safu zinazokabilina katika masuala mengi hususan katika migogoro ya eneo la magharibi mwa Asia na kaskazini mwa Afrika. Katika miaka ya hivi karibuni Imarati imekuwa ikishiriki katika mipango yote iliyo dhidi ya Uturuki, ama kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja. Katika uwanja huu tunaweza kuashiria ushiriki wa Imarati katika jaribio la mapinduzi dhidi ya serikali ya Uturuki tarehe 15 Julai mwaka 2016; tukio ambalo limeacha taathira kubwa sana katika uhusiano wa nchi hizo mbili.