"Arab League ni wenzo tu wa nchi za wasaliti"
Harakati ya Wananchi kwa ajili ya Ukombozi wa Palestina imesema kuwa, Jumuiya ya Nchi za Kiarbu (Arab League) ni wenzo tu unaotumiwa na nchi za wasaliti kwa ajili ya kufanikisha malengo ya kisaliti.
Shirika la habari la FARS limeinukuu harakati hiyo ikisema hayo leo Alkhamisi na kuongeza kuwa kitendo cha Jumuiya ya Nchi za Kiarabu cha kushindwa kupasisha azimio la kulaani kuweka uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel ni kitu kinachopaswa kulaani na kusisitiza kuwa, Arab League imefika mwisho wake na imeonesha kivitendo kuwa haiguswi kivyovyote na masuala ya ulimwengu wa Kiarabu baada ya kushindwa kulaani kitendo cha Umoja wa Falme za Kiarabu cha kutangaza rasmi uhusiano wake wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Harakati ya wananchi ya Ukombozi wa Palestina imesema kwa uwazi kwamba msimamo wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ni wa kiburi, kijeuri na wa kuzichochea nchi nyingine zifuate mkumbo wa Umoja wa Falme za Kiarabu wa kutangaza uhusiano wao rasmi na utawala wa Kizayuni.
Taarifa ya harakati hiyo imekitaka Chama cha Ukombozi wa Palestina PLO na makundi mengine yote ya kitaifa ya Palestina kusimama imara kupinga msimamo huo wa Arab League na kutokubali hata kidogo usaliti wa baadhi ya nchi za Kiarabu wa kuwa na uhusiano wa kawaida na wavamizi wa Quds.
Jana Jumatano, baadhi ya nchi za Kiarabu zilipinga muswada uliowasilishwa na Palestina katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu wa kutaka kulaaniwa hatua ya Imarati ya kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.