Ismail Haniya: Historia haitawahurumia walioanzisha uhusiano na utawala wa Israel
Ismail Haniya Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesema historia haitazihurumia hata kidogo nchi za Kiarabu kutokana na hatua ya kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel na mataifa nayo hayatasahau kitendo hicho.
Kiongozi huyo wa Hamas pia amewafahamisha watawala wa Umoja wa Falme za Kiarabu na Bahrain kuwa wamepata hasara katika mapatano yao na Israel na kuongeza kuwa, lengo kuu la Israel ni kuwa na vituo vya kijeshi na kiuchumi karibu na Iran.
Ismail Haniya amesema harakati ya Hamas iko tayari kukabiliana na hujuma yoyote ile ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Ghaza na kuongeza kuwa: "Vita vyovyote katika mustakabali vitamsababishia adui hasara kubwa."
Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas pia ameashiria mpango wa kubadilishana mateka na kusema ujumbe wa Misri umeufahamisha utawala wa Kizayuni kuhusu masharti ya Hamas na kwa sasa Hamas inasubiri jibu.
Umoja wa Falme za Kiarabu na Bahrain baada ya kufikia mapatano na utawala wa Kizayuni wa Israel unaoikalia Quds kwa mabavu; tarehe 15 mwezi Septemba mwaka huu zilisaini huko White House mapatano ya kuanzisha uhusiano rasmi na utawala huo wa Kizayuni. Tukio hilo lilihudhuriwa na Rais Donald Trump wa Marekani na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.