Jordan yasisitiza tena kuundwa nchi huru ya Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i64118-jordan_yasisitiza_tena_kuundwa_nchi_huru_ya_palestina
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan ametaka ipatikane amani ya kweli na kiuadilifu itakayodhamini kuundwa nchi huru ya Palestina.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Oct 19, 2020 23:00 UTC
  • Ayman As-Safadi
    Ayman As-Safadi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan ametaka ipatikane amani ya kweli na kiuadilifu itakayodhamini kuundwa nchi huru ya Palestina.

Ayman As-Safadi ameyasema hayo katika mkutano na waandishi wa habari aliofanya pamoja na mgeni wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Kuwait mjini Amman, ambapo mbali na kukosoa mapatano ziliyofanya Imarati na Bahrain ya kuanzisha uhusiano rasmi na utawala wa Kizayuni wa Israel, amesisitiza kwa mara nyingine kuundwa nchi huru ya Palestina.

As-Safadi ametoa kauli hiyo wakati siku ya Jumapili ujumbe wa pamoja wa Marekani na Israel ulielekea Bahrain kukamilisha mchakato wa kusaini hati rasmi ya kuanzishwa uhusiano kati ya nchi hiyo na utawala wa Kizayuni.

Katika safari hiyo, ujumbe huo wa pamoja wa Marekani na utawala haramu wa Israel uliongozwa na Waziri wa Fedha wa Marekani Steven Mnuchin na Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel  Alon Ushpiz na  mshauri wa usalama wa taifa wa utawala huo wa Kizayuni Meir Ben-Shabbat.

Kabla ya safari hiyo ya siku ya Jumapili ya ujumbe wa pamoja wa Marekani na Israel huko Bahrain, wananchi wa nchi hiyo walifanya maandamano ya kupinga kuanzishwa uhusiano na kusainiwa rasmi mkataba wa mapatano kati ya nchi yao na utawala wa Kizayuni.

Jumapili usiku pia wananchi wa Bahrain walikusanyika katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo wakibeba maberamu yaliyoandikwa: "Wazayuni tokeni nchini mwetu... makubaliano yenu ni batili" na "makubaliano yote na Wazayuni ni batili na utawala wa Bahrain hauna uhalali wa kisiasa" ili kuonyesha upinzani wao kwa hatua ya utawala wa Aal Khalifa ya kuanzisha uhusiano rasmi na Israel.../