UN: Inabidi utawala wa Kizayuni uchukuliwe hatua
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i64338-un_inabidi_utawala_wa_kizayuni_uchukuliwe_hatua
Ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Palestina ameitaka jamii ya kimataifa iuchukulie hatua utawala wa Kizayuni wa Israel kutokana na jinai zake dhidi ya Wapalestina.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 31, 2020 04:07 UTC
  • UN: Inabidi utawala wa Kizayuni uchukuliwe hatua

Ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Palestina ameitaka jamii ya kimataifa iuchukulie hatua utawala wa Kizayuni wa Israel kutokana na jinai zake dhidi ya Wapalestina.

Quds Press imemnukuu Michael Lynk akitoa mwito huo leo Jumamosi na kuongeza kuwa, hatua ya Baraza la Mawaziri la utawala wa Kizayuni ya kupasisha ujenzi wa nyumba 5,000 katika ardhi walizoporwa Wapalestina ni ukiuakaji wa wazi wa sheria za kimataifa na inabidi jamii ya kimataifa iichukulie hatua Israel.

Amesema, katika mwaka huu wa 2020 utawala wa Kizayuni umepasisha ujenzi wa zaidi ya nyumba 12,000 za walowezi wa Kizayuni.

Ikumbukwe kuwa, wakati baadhi ya nchi za Kiarabu zilipojiingiza kwenye wimbi la kutangaza uhusiano wa kawaida na Wazayuni, zilidai kuwa zimefanya hivyo ili kuizuia Israel isipore ardhi zaidi za Wapalestina. 

Kutangaza baadhi ya nchi za Kiarabu uhusiano na Israel hakujazuia ujenzi wa viongoji vya walowezi wa Kizayuni na kuporwa Wapalestina ardhi zao

 

Hata hivyo viongozi wa utawala wa Kizayuni walikanusha haraka madai hayo na kusema, kutangazwa uhusiano wa kawaida baina ya Israel na nchi za Kiarabu hakutauzuia utawala huo kuendelea na siasa zake za kupora ardhi za Wapalestina na kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni.

Matamshi ya karibuni kabisa ni ya mwakilishi wa rais wa Marekani wa masuala ya Asia Magharibi, Avi Berkowitz, ambaye ameiambia redio moja ya utawala wa Kizayuni kuwa, mpango wa kumegwa sehemu ya ardhi za Wapalestina za Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan na kuunganishwa na ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni na ambazo zimepachikwa jina bandia la Israel, bado upo pale pale.