Uingereza na Palestina; miaka 103 baada ya Azimio la Balfour
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i64419-uingereza_na_palestina_miaka_103_baada_ya_azimio_la_balfour
Juzi Jumatatu tarehe Pili Novemba ilisadifiana na kutimia mwaka wa 103 wa Azimio la Balfour.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Nov 04, 2020 03:14 UTC
  • Uingereza na Palestina; miaka 103 baada ya Azimio la Balfour

Juzi Jumatatu tarehe Pili Novemba ilisadifiana na kutimia mwaka wa 103 wa Azimio la Balfour.

Baada ya kupita miaka 103 tangu lilipopitishwa Azimio la Balfour, swali linaloulizwa hivi sasa ni je, Uingereza, ilikuwa na nafasi gani katika vuta nikuvute ya mgogoro wa Palestina na Israel?

Uingereza ndilo dola la kwanza la Magharibi ambalo lilichangia kuasisiwa kwa utawala wa Kizayuni wa Israel. Kwa mara ya kwanza, uchangiaji na uungaji mkono huo ulichukua sura rasmi kupitia Azimio la Balfour. Azimio la Balfour lililopitishwa tarehe Pili Novemba 1917 lilifungua njia ya kuundwa utawala bandia wa Kizayuni kwa uungaji mkono wa dola la kikoloni la Uingereza katika ardhi ya watu wa Palestina.

Azimio la Balfour lilikuwa ni barua ambayo mnamo mwaka huo wa 1917, waziri wa mambo ya nje wa Uingereza wakati huo Arthur James Balfour alimwandikia mwanasiasa na mbunge wa bunge la Uingereza mwenye asili ya Kiyahudi Walter Rothschild. Katika barua hiyo, Balfour alitangaza msimamo wa serikali ya Uingereza wa kuunga mkono kuasisiwa kile kilichotajwa kuwa ni "makazi ya kitaifa kwa ajili ya Mayahudi" katika ardhi ya Palestina.

Uungaji mkono wa Uingereza kwa utawala wa Kizayuni uliendelea kwa sura tofauti hata baada ya kuundwa utawala huo haramu, ukiwemo wa kuwapatia silaha Wazayuni, kuwaunga mkono kisiasa na kijeshi na kufumbia macho jinai ambazo utawala huo unawafanyia Wapalestina na vilevile kuyapigia kura ya veto maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya Tel Aviv.

Swali jengine linaloulizwa ni je, hivi sasa Palestina iko katika hali gani baada ya miaka 103 ya Azimio la Balfour?

Arthur James Balfour

Leo Palestina inakabiliwa na hali mbaya ya mashinikizo kuliko wakati wowote ule. Upande mmoja kuna Marekani, ambayo imezindua mpango wake wa kibaguzi wa 'Muamala wa Karne' usiozingatia kitu chochote isipokuwa manufaa na maslahi ya utawala haramu wa Israel. Na upande mwingine kuna nchi za Kiarabu, ambazo kwa miongo kadhaa tangu lilipopitishwa Azimio la Balfour zilikuwa zikiihami na kuiunga mkono Palestina na hata zikaingia vitani mara nne kupambana na utawala wa Kizayuni, lakini leo zimebadilika kwa kuamua kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo ghasibu, ambapo kwa kufanya hivyo, si tu zimeiacha mkono Palestina, bali zimegeuka kuwa waungaji mkono wa jinai wanazotendewa wananchi madhulumu wa ardhi hiyo.

Katika hali na mazingira haya, mashinikizo na jinai za utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina zimeongezeka. Kubomolewa nyumba za Wapalestina, kujengwa vitongoji haramu vya walowezi wa Kizayuni, kuuliwa na kujeruhiwa Wapalestina wasio na hatia, ukatili dhidi ya mateka wa Kipalestina na kuendelezwa mzingiro dhidi ya Ukanda wa Gaza ni miongoni mwa jinai ambazo utawala wa Kizayuni unaendelea kuwatendea Wapalestina.

Na suali la mwisho la kujiuliza ni je, Uingereza ina sera gani kuhusiana na hali ya sasa ya Palestina?

Kuhusiana na suala hilo, Naser Abu Sharif, mwakilishi wa harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina hapa mjini Tehran anasema: "Kidhahiri, Uingereza inapinga kwa kiwango fulani mpango wa Muamala wa Karne na inatetea mpango wa kuundwa nchi mbili, lakini ukweli ni kwamba Uingereza haijachukua hatua yoyote ya maana na ya kivitendo katika suala hilo, na kama kuna kitu imefanya ni kutoa kauli na maneno matupu kwa sababu imeikabidhi mambo yote Marekani." 

Hali ya ardhi ya Palestina ilivyokuwa 1917 mpaka ilivyo hivi sasa

Ijapokuwa Uingereza imeamua kufuata sera hiyo, lakini ndani ya nchi hiyo kuna asasi na jumuiya kadhaa ambazo zinaishinikiza serikali ya London iache kuifuata Marekani katika kila sera na badala yake ipingane na Washington na kuwa na misimamo huru katika baadhi ya siasa na sera zake. Miongoni mwa asasi hizo ni jumuiya za kutetea haki za binadamu, baadhi ya vyama vya siasa, wahadhiri wa vyuo vikuu, shakhsia wa kisiasa na baadhi ya wanafasihi na wanafikra ambao wanataka Uingereza iususie utawala wa Kizayuni. Hata hivyo serikali ya London haijali upinzani huo na badala yake inaendelea kuuunga mkono utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina ili ibaki kuwa mshirika muhimu wa jinai zinazofanywa kila uchao na utawala huo ghasibu dhidi ya wananchi hao madhulumu.../