Palestina yalitaka Baraza la Usalama kukabiliana na jinai za walowezi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i65415-palestina_yalitaka_baraza_la_usalama_kukabiliana_na_jinai_za_walowezi
Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Palestina imetoa taarifa inayolitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuchukua hatua za kukomesha jinai za walowezi wa Kizayuni huko Palestina.
(last modified 2026-08-14T10:24:44+00:00 )
Dec 26, 2020 11:02 UTC
  • Palestina yalitaka Baraza la Usalama kukabiliana na jinai za walowezi

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Palestina imetoa taarifa inayolitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuchukua hatua za kukomesha jinai za walowezi wa Kizayuni huko Palestina.

Taarifa hiyo sambamba na kuashiria jinai za walowezi wa Kizayuni imesisitiza pia kuwa, hujuma na uvamizi wa walowezi hao dhidi ya wananchi wa Palestina haufanyiki kwa lengo la kuzusha hofu, wahaka na maudhi tu, bali ni mipango ya kikoloni na kujitanua inayolenga kupora zaidi ardhi za Palestina.

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Palestina imelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutekeleza majukumu yake ipasavyo hususan kuhusiana na kuheshimiwa sheria za kimataifa na misingi ya haki za binadamu.

Kadhalika Palestina imekitaka chombo hicho cha kimataifa kuhakikisha azimio nambari 2334 la Umoja wa Mataifa linaloharamisha ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni huko Palestina na jinai zao linatekelezwa kikamilifu.

Ujenzi wa vitongoji haramu vya walowezi wa Kizayuni huko Palestina

 

Jumuiya mbalimbali za kieneo na kimataifa zimekuwa zikieleza upinzani wao dhidi ya ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina na hata kuutaka utawala ghasibu wa Israel usitishe ujenzi huo.

Hata hivyo uungaji mkono wa Marekani kwa Israel umekuwa ukiupa kiburi utawala huo cha kuendelea na siasa zake za kidhalimu dhidi ya Wapalestina bila ya kujali hasira za walimwengu.

Ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni, kubomolewa nyumba za Wapalestina, kuporwa ardhi zao, kufanywa wakimbizi na kufukuzwa katika maeneo yao ni miongoni mwa jinai kubwa zinazofanywa kila leo na utawala wa Kizayuni wa Israel.