2020; ulikuwa mwaka mweusi kwa raia katika eneo la Asia Magharibi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i65642-2020_ulikuwa_mwaka_mweusi_kwa_raia_katika_eneo_la_asia_magharibi
Mwaka 2020 umemalizika hivi majuzi, lakini tukitupia jicho kwa haraka haraka matukio yaliyogonga vichwa vya habari katika mwaka huo tunaona kuwa, wananchi wa eneo la Asia Magharibi walikuwa wahanga wakuu wa matukio yaliyoshuhudiwa katika eneo hili.
(last modified 2025-10-31T09:05:42+00:00 )
Jan 08, 2021 02:40 UTC
  • 2020; ulikuwa mwaka mweusi kwa raia katika eneo la Asia Magharibi

Mwaka 2020 umemalizika hivi majuzi, lakini tukitupia jicho kwa haraka haraka matukio yaliyogonga vichwa vya habari katika mwaka huo tunaona kuwa, wananchi wa eneo la Asia Magharibi walikuwa wahanga wakuu wa matukio yaliyoshuhudiwa katika eneo hili.

Katika mwaka uliopita wa 2020, virusi vya Corona vilikuwa chanzo kikuu cha vifo na maafa ulimwenguni likiwemo eneo la Asia Magharibi.

Pamoja na hayo, eneo la Asia Magharibi lilishuhudia raia wengi wakiaga dunia mwaka jana kutokana na machafuko na vitendo vya utumiaji mabavu vilivyotwishwa eneo hili. Hali hiyo iliufanya mwaka jana kuwa mwaka mweusi kwa wananchi. Takwimbu mbalimbali zilizotolewa na asasi na jumuiya tofauti zinathibitisha hilo.

Brigedia Jenerali Yahya Saree, msemaji wa majeshi ya Yemen ametangaza kuwa, muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia ulifanya mashambulio 8,888 katika mwaka uliopita wa 2020 dhidi ya miji 13 ya Yemen ambapo mashambulio 410 kati ya hayo yalitekelezwa kwa kutumia ndege zisizo na rubani (drone) na kupelekea mamia ya raia kuuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa sambamba na kusababisha hasara na uharibifu mkubwa dhidi ya mali za watu.

Kituo cha haki za Binadamu cha B’Tselem cha Israel kimesema katika ripoti yake kwamba: Mwaka uliopita Wapalestina 27 waliuawa shahidi wakiwemo watoto 7 baada ya kupigwa risasi na wanajeshi wa Israel.

Mlipuko katika Bandari ya Beirut Agosti4, 2020

 

Mlipuko wa tarehe 4 Agosti mwaka jana katika Bandari ya Beirut Lebanon ulipelekea watu takribani 200 kuuawa na wengine zaidi ya 7,000 kujeruhiwa. Maandamano na vurugu za ndani nchini Iraq mwaka uliopita zilisababisha zaidi ya watu 400 kuuawa na wengine 7,000 kujeruhiwa. Nchini Syria hakuna takwimu za uhakika kuhusiana na mauaji dhidi ya raia katika mwaka uliopita, lakini ripoti mbalimbali zinaashiria kuwa, maelfu ya watu waliuawa katika vita vya ugaidi nchini humo.

Fauka ya hayo, kuuawa na kujeruhiwa raia katika baadhi ya nchi za Asia Magharibi katika mwaka uliopita, kulisababisha hasara kubwa za kimaada.  Nchini Yemen, Lebanon na Palestina idadi kubwa ya watu walipoteza nyumba na kazi zao na kulazimika kuwa wakimbizi. Kwa mfano, Kituo cha Haki za Binadamu cha Israel kimetangaza katika ripoti yake kwamba, mwaka uliopita, majengo 729 ya Wapalestina yalibomolewa kwa kisingizio cha kutokuwa na kibali cha ujenzi, na hivyo kuwafanya Wapalestina zaidi ya 6,000 kuwa wakimbizi wakiwemo watoto 519.

Saudia imeendelea kufanya mauaji dhidi ya raia nchini Yemen 

 

Haya ni matukio machache ya hasara, madhara na masaibu waliyokumbana nayo raia katika baadhi ya nchi za Asia Magharibi kutokana na hujuma na machafuko ya kulazimishwa dhidi ya nchi zao. Aidha tunaweza kuongezea katika orodha hiyo, kamatakamata iliyofanywa katika baadhi ya maeneo hususan Palestina inayokaliwa kwa mabavu na huko Saudi Arabia na wagonjwa walioaga dunia huko katika Ukanda wa Gaza na Yemen kutokana na kukosa dawa kufuatia mzingiro, au watu ambao wameaga dunia kwa njaa hususan nchini Yemen.

Yumkini baadhi ya nchi za Kiafrika nazo zikawa zilikumbwa na hali hii mwaka uliopita, lakini machafuko na vitendo vya utumiaji mabavu Asia Mgharibi ni jambo ambalo wananchi wa eneo hili walitwishwa na kupandikiziwa. Vita na hujuma ya kijeshi ya muungano vamizi wa Saudia dhidi ya wananchi wa Yemen siyo jambo la ndani, bali ni jambo kutoka nje ambalo wananchi wa nchi hiyo masikini walitwishwa.

Mzingiro, vita na utumiaji mabavu katika Ukanda wa Gaza katu si mambo ya ndani, bali ni matokeo ya vitendo vua kujitanua na uvamizi wa utawala haramu wa Israel. Hata nchini Syria, Iraq na Lebanon kwa asilimia kubwa matukio yaliyozikumba nchi hizo yalipangwa na kupikwa na watu kutoka nje.

Magaidi wa Daesh ambao wamesambaratishwa nchini Syria

 

Sababu kuu ya kuanza na kuibuka vitendo vya kutwishwa eneo la Asia Magharibi vinahusiana na uwepo wa utawala bandia katika eneo hili. Madola ya Magharibi hususan Marekani yanakaribisha kwa mikono miwili kutokea machafuko ndani ya nchi za Asia Magharibi hususana mataifa ambayo yana ukaribu na mhimili wa muqawama wakiamini kwamba, hilo linadhamini usalama wa Israel.

Kwa maneno mengine ni kuwa, kuchukizwa Marekani, utawala haramu wa Israel na Saudia na suala la kuimarika na kupata nguvu muqawama ndio mambo yaliyozisukuma tawala hizo kuandaa mazingira ya kupandikiza machafuko na vitendo vya utumiaji mabavu ndani ya mataifa hayo.

Mlolongo wa machafuko ni aina nyingine ya mzozo wa kisiasa kwa ajili ya kukabiliana na muqawama na katika hili, siyo tu kwamba, kuheshimu haki za binadamu ni jambo lisilo na nafasi kabisa, bali kimsingi kushadidisha machafuko dhidi ya raia ni wenzo unaotumiwa kwa ajili ya kuushinikiza mhimili wa muqawama.

Mwenendo huu, umeongezeka sana katika miaka ya hivi karibuni hususan katika kipindi cha utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani, kwani kwa mtazamo wa siasa za Trump si tu kwamba, suala la haki za binadamu halina nafasi yoyote, bali chuki na utumiaji mabavu ndio mambo yanayotawala katika sera zake.