Ishara za mabadiliko katika siasa za kieneo za Saudi Arabia
Sambamba na kumalizika kipindi cha uongozi wa Donald Trump nchini Marekani, kumedhihirika bayana ishara za mabadiliko katika siasa na sera za kieneo za Saudi Arabia.
Utawala wa Aal Saud ulitumia gharama kubwa ukifanya juhudi za kunufaika na karata ya kuweko madarakani serikali ya Donald Trump katika siasa zake za kieneo. Licha ya kuwa, vita vya Saudia na washirika wahe dhidi ya Yemen vilianza katika kipindi cha utawala wa Rais Barack Obama, lakini serikali Trump baada ya kuingia madarakani ilifumbia macho vitendo vyote vya ukiukaji wa haki za binadamu vya Saudia nchini Yemen, na hivyo kuisafishia njia Riyadh ya kuendelea na vita hivyo pasi na wasiwasi wowote ule.
Miezi sita tu baada ya serikali ya Trump kuingia madarakani, utawala wa Saudia uliingia katika mzozo na mvutano na Qatar, na ikiwa na lengo la kuifanya Doha ibadilishe sera zake za kigeni ilishirikiana na mataifa mengine ya Kiarabu ya Bahrain, Misri na Imarati kuiwekea mzingiro nchi hiyo sanjari na kukata kabisa uhusiano nayo.
Mvutano wa Saudia na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nao licha ya kuwa ulianza katika kipindi cha utawala wa Barack Obama na baada ya Saudia kumnyonga Sheikh Nimr Baqir al-Nimr, lakini ukweli ni kuwa, Riyadh ilikuwa na nafasi kubwa katika mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa ya Washington dhidi ya Tehran. Katika kipindi hiki, uhusiano wa Riyadh na Tehran umeondoka kabisa katika anga ya ushindani na kuingia katika hatua ya chuki na hasama.
Katika kipindii cha uongozi wa Trump, Saudia ilitumbukia pia katika mzozo na mgogoro na Uturuki. Mzozo huo ulijikita zaidi katika mambo matatu ya mashinikizo dhidi ya Qatar, kuitambua Harakati ya Ikhwan al-Muslimin kuwa ni kundi la kigaidi na mauaji ya kikatili dhidi ya mwandishi habari Jamal Khashoggi aliyeuawa katika ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul. Masuala hayo kwa hakika yalipelekea kuibuka mpasuko katika uhusiano wa pande mbili na hali ya kila mmoja kujaribu kuwa mbali na mwenziwe.
Hizi kwa hakika ni changamoto muhimu zilizokuweko katika sera za kigeni za Saudia katika kipindi cha utawala wa miaka minne wa Donald Trump, ambapo serikali ya Riyadh ikipata himaya na uungaji mkono wa serikali ya Trump haikuwa na hofu wala wasiwasi katika mzozo wa uhusiano wake na mataifa mengine au hata na mataifa yenye nguvu katika eneo la Asia Magharibi.
Lakini hivi sasa hali inaonekana kuwa tofauti hasa kutokana na kumalizika kipindi cha utawala wa Trump aliyekuwa akiingikia kifua Riyadh. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana hivi sasa kunaonekana ishara mpya katika siasa na sera za kigeni za Saudi Arabia, jambo ambalo linaonyesha kuweko mabadiliko tarajiwa katika sera za kieneo za Riyadh.
Ibrahim Mottaqi, mhadhiri wa Chuo Kikuu anaamini kuwa, Saudia inakusudia kupunguza changamoto za sera zake za kigeni, kwani inaamini kuwa, serikali ya Rais mpya wa Marekani Joe Biden haitakuwa kama ilivyokuwa serikali ya Trump kwa utawala wa Aal Saud.
Katika hatua ya awali, Saudia imelazimika kufanya mageuzi katika sera zake za kigeni na kuchukua hatua katika mkondo wa kuupatia ufumbuzi mzozo baina yake na Qatar. Licha ya kuwa, kumalizika mvutano baina yake na Qatar kwa namna fulani ni pigo kwa haiba ya Riyadh, lakini kuhitimisha mgogoro huo kuna gharama ndogo ikilinganishwa na mgogoro wa Yemen na mvutano baina yake na Uturuki. Qatar ni nchi ya Kiarabu iliyo jirani na Saudia.
Inaonekana kuwa, serikali ya Riyadh imeonyesha pia kuwa iko tayari kuhitimisha hitilafu zilizoko baina yake na Uturuki. Qatar ina ukuruba na uhusiano mzuri na Uturuki na imejitokeza na kutoa pendekezo la kuwa mpatanishi wa Riyadh na Ankara, pendekezo ambalo kidhahiri linaonekana tayari limekubaliwa na pande mbili husika. Kwa muktadha huo basi, tutaraji kuona yakifanyika mazungumzo baina ya Saudi Arabia na Uturuki kwa ajili ya kuzitafutia ufumbuzi hitilafu zilizopo baina yao.
Endapo hilo litatokea, bado ni Saudia ndiyo ambayo kimsingi itakuwa imelegeza kamba ya misimamo yake ya huko nyuma kuhusiana na Uturuki; kwani Riyadh ilikuwa ikitaka Ankara iondoke Qatar takwa ambalo halijatekelezwa. Aidha Saudia ilikuwa ikiitaka Uturuki iache kuiunga mkono Harakati ya Ikhwan al-Muslimin jambo ambalo nalo halijatekelezwa.
Kuna changamoto nyingine mbili katika sera za kigeni za Saudi Arabia ambazo hadi sasa hakuna ishara za kutaka kuzimaliza. Hata hivyo uwezekano wa Saudia kuzipatia ufumbuzi changamoto hizo hivi sasa ni mkubwa ikilinganishwa na kipindi cha utawala wa Trump.
Hadi sasa hakuna ishara zozote za Saudia kutaka kuhitimisha vita dhidi ya Yemen au kuhuisha uhusiano wake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hata hivyo hivi karibuni Faisal bin Farhan al-Saud, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Saudi Arabia alifanya safari mjini Moscow ambako alikutana na kufanya mazungumzo na Sergei Lavrov, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia. Kuna uwezekano kwamba, katika safari yake hiyo Faisal aliwasilisha kwa nchi hiyo ujumbe wa Riyadh kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kuna uwezakano pia kwamba, Russia imetangaza utayari wa kuwa mpatanishi wa Riyadh na Tehran.
Majimui ya matukio haya kabla ya kila kitu yanaweka wazi nukta hii kwamba, sera za kigeni za Saudia zina mfungamano mkubwa na nafasi na matukio ya nje yaani ya Marekani, na katu hazifuati misingi thabiti na ya kudumu.