Al Barghouthi: Uchaguzi ni utangulizi wa kufikiwa umoja wa kitaifa Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i66436-al_barghouthi_uchaguzi_ni_utangulizi_wa_kufikiwa_umoja_wa_kitaifa_palestina
Katibu Mkuu wa Vuguvugu la Ubunifu wa Kitaifa la Palestina amesisitiza kuwa uchaguzi ni utangulizi wa kuhitimishwa mpasuko na mgawanyiko na kufikiwa umoja wa kitaifa wa Palestina.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 04, 2021 00:56 UTC
  • Al Barghouthi: Uchaguzi ni utangulizi wa kufikiwa umoja wa kitaifa Palestina

Katibu Mkuu wa Vuguvugu la Ubunifu wa Kitaifa la Palestina amesisitiza kuwa uchaguzi ni utangulizi wa kuhitimishwa mpasuko na mgawanyiko na kufikiwa umoja wa kitaifa wa Palestina.

Mustafa al Barghouthi amesema, kungali kuna baadhi ya mambo ambayo Wapalestina wanahitilafiana, kwa hiyo inapasa yatatuliwe ili kuweza kuhakikisha unaitishwa uchaguzi safi na unaokubalika.

Al Baroghouthi ameeleza bayana: "tunapinga uingiliaji wa nchi yoyote ile katika masuala ya ndani ya Palestina, kwa sababu nchi hiii inahitaji kuwa huru kikamilifu kwa ajili ya mchakato wa kidemokrasia na inapasa wananchi wa Palestina wanufaike na haki yao ya kimaumbile waliyoikosa kwa muda wa miaka 14 na hivyo kumchagua kwa uhuru kamili mtu anayefaa kwa uongozi."

Katibu Mkuu wa Vuguvugu la Ubunifu wa Kitaifa la Palestina amesisitiza kuwa, kabla ya jambo jengine lolote lile, lengo kuu la uchaguzi wa Palestina ni kuleta mabadiliko, na yanahitajika mabadiliko; kwa sababu wananchi wako taabani kutokana na hali iliyopo hivi sasa pamoja na matatizo ya kisiasa na kijamii; na wanataka aina fulani ya mabadiliko na kutumiwa mbinu mpya katika kulishughulikia suala la kitaifa na masuala mengine ya kijamii.

Mahmoud Abbas

Kwa mtazamo wa shakhsia huyo wa Palestina, inapasa Wapalestina wawe na stratejia ya kitaifa itakayochukua nafasi ya hatua za huko nyuma zilizofeli hususan Mkataba wa Oslo; na wala hakuna faida yoyote ya kuwa na matumaini juu ya mazungumzo hata baada ya kuingia madarakani Joe Biden nchini Marekani.

Kwa mujibu wa agizo lililotolewa na Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, uchaguzi wa bunge la Palestina utafanyika tarehe 22 Mei na uchaguzi wa rais utafanyika tarehe 31 Julai mwaka huu. Chaguzi hizo zitafanyika kwa mara ya kwanza katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu baada ya kupita miaka 15.../