Jeshi la Syria lakomboa madaktari kutoka mikononi mwa Daesh
Jeshi la serikali ya Syria limefanikiwa kukomboa hospitali moja katika mji wa Dayr al Zawr wa mashariki mwa nchi hiyo kutoka katika makucha ya genge la kitakfiri la Daesh.
Shirika linalodaiwa la kuangalia haki za binadamu nchini Syria lenye makao yake nchini Uingereza lilitangaza habari hiyo jana na kuongeza kuwa, wanajeshi wa serikali ya Syria wamefanikiwa kuikomboa Hospitali ya Assad baada ya kupambana vikali na wanamgambo wa Daesh.
Nalo shirika la habari la Russia RIA limeinukuu duru moja katika uwanja wa ndege wa Dayr al Zawr ikisema kuwa, jeshi la Syria limefanikiwa pia kuzima shambulio la magaidi wa Daesh kwenye hospitali hiyo.
Wakati huo huo duru moja ya kijeshi ambayo haikutaka kutaja jina lake imeliambia shirika la habari la China la Xinhua kwamba, jeshi la Syria limefanikiwa kuwakomboa madaktari na wauguzi kadhaa waliokuwa wametekwa nyara na magaidi katika hospitali hiyo.
Kundi la kigaidi la Daesh linadhibiti zaidi ya nusu ya mji wa Dayr al Zawr, na serikali inashindwa kufanya mashambulizi ya kiholela kutokana na magaidi wa Daesh kuwashikilia mateka watu wapatao laki mbili katika mji huo. Mkoa wa Dayr al Zawar unaunganisha ngome ya Daesh ya Raqqah na maeneo yanayodhibitiwa na genge hilo katika nchi jirani ya Iraq.