Al- Muallem: Watakaoivamia Syria watarejeshwa makwao wakiwa kwenye majeneza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i721-al_muallem_watakaoivamia_syria_watarejeshwa_makwao_wakiwa_kwenye_majeneza
Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria Walid al-Muallem amesema watakaoivamia ardhi ya Syria watarejeshwa makwao wakiwa kwenye majeneza.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 06, 2016 11:31 UTC
  • Syrian's Foreign Minister
    Syrian's Foreign Minister

Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria Walid al-Muallem amesema watakaoivamia ardhi ya Syria watarejeshwa makwao wakiwa kwenye majeneza.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Damascus, al- Muallem amesema pande nyengine katika mazungumzo ya amani ya Syria hazikuwa na nia ya kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa nchi hiyo kupitia mazungumzo baina ya Wasyria wenyewe. Amesema kupiga hatua jeshi la Syria katika medani za vita ndiyo sababu iliyowafanya wapinzani wa serikali wanaoungwa mkono na Saudi Arabia kujiondoa kwenye mazungumzo ya Geneva. Amesema mara baada ya kukombolewa miji ya Nubl na Al-Zahraa mrengo wa Riyadh wa ujumbe wa wapinzani ulijiondoa kwenye mazungumzo ya Geneva.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria amesisitiza kuwa shambulio lolote la ardhini litakalofanywa ndani ya ardhi ya Syria bila ya idhini ya serikali ya nchi hiyo litahesabiwa kuwa ni uvamizi; na wale watakaoivamia Syria watarudi makwao wakiwa kwenye majeneza.

Duru ya tatu ya mazungumzo ya amani ya Syria ilianza tarehe 29 Januari mjini Geneva lakini mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Syria Staffan de Mistura, aliakhirisha mazungumzo hayo siku ya Jumatano iliyopita ya tarehe 3 Februari na kutangaza kuwa yataendelea tena tarehe 25 mwezi huu.../