Pakistan yataka kuwajibishwa India kwa jinai dhidi ya wakazi wa Kashmir
-
Imran Khan
Pakistan imeitaka jamii ya kimataifa kuiwajibisha na kuibebesha dhima New Delhi, kwa kukanyaga haki za binadamu katika eneo linalodhibitiwa na India huko Jammu na Kashmir.
Mwito huo umetolewa leo Alkhamisi na Waziri Mkuu wa Pakistan, Imran Khan kwa mnasaba wa kuwadia miaka miwili tangu India iliunganishe eneo hilo na ardhi yake.
Khan amesema licha ya New Delhi kuchukua hatua hiyo iliyo kinyume cha sheria mnamo Agosti 5 mwaka 2019, lakini imeshindwa kuvunja azma na irada ya wananchi wa Kashmir.
Waziri Mkuu wa Pakistan amesema kwa miaka na miaka sasa, India imeweka maelfu ya askari wa jeshi lake katika maeneo ya Kashmir na katika kipindi cha miongo mitatu ya karibuni imeua maelfu ya watu katika eneo hilo la Waislamu.
India na Pakistan zinazozana na kuhitilafiana kwa miongo kadhaa sasa kuhusu umiliki wa eneo la Kashmir, na hitilafu hizo zimeifanya kila moja kati ya nchi hizo mbili itumie nguvu na mabavu kwa ajili ya kulidhibiti eneo hilo.
Wananchi Waislamu wa Kashmir wanataka kutekelezwa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalohusiana na uitishaji kura ya maamuzi ya kuainisha hatima ya eneo hilo, lakini serikali ya India inapinga utekelezwaji wa azimio hilo