Hamas yawataka Wapalestina wajitayarishe kuutetea Msikiti wa al Aqsa
(last modified Sat, 09 Oct 2021 07:56:29 GMT )
Oct 09, 2021 07:56 UTC
  • Hamas yawataka Wapalestina wajitayarishe kuutetea Msikiti wa al Aqsa

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imewataka Wapalestina wajitayarishe kwa ajili ya kuutetea Msikiti wa al Aqsa bila ya kujali uamuzi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wa kusitisha azma yake ya kuruhusu ibada ya Mayahudi katika eneo hilo tukufu.

Ismail Ridhwan ambaye ni miongoni mwa maafisa wa ngazi za juu wa Hamas amesema kuwa, Msikiti wa al Aqsa ni kibla cha kwanza cha Waislamu na kwamba utawala bandia wa Israel kamwe hautafanikiwa katika njama zake za kupotosha historia ya eneo hilo. 

Ridhwan amesema Hamas haitauruhusu utawala huo kuzusha mgogoro mpya katika Msikiti wa al Aqsa na imewataka wakazi wa mji wa Quds na ardhi zilizokaliwa kwa mabavu mwaka 1948 kujitayarisha kwa ajili ya kulinda kibla cha kwanza cha Waislamu.  

Mahakama ya utawala wa Kizayuni wa Israel Jumanne iliyopita ilitoa hukumu ya aina yake ikiwaruhusu Wayahudi kufanya ibada katika viwanja vya Msikiti wa al Aqsa. Uamuzi huo umepingwa vikali na makundi ya kupigania uhuru ya Palestina na nchi nyingi za Kiislamu. 

Kufuatia upinzani huo mkali Polisi ya Israel iliitaka mahakama kuu katika mji wa Quds (Jerusalem) kutazama upya hukumu hiyo. Ijumaa ya jana vyombo vya habari viliripoti kuwa mahakama hiyo imelegeza kamba na kutengua uamuzi wa kuwaruhusu Wayahudi kutekeleza ibada zao katika viwanja vya Msikiti wa al A qsa. 

Kabla ya hapo makundi ya mapambano ya ukombozi wa Palestina yalikuwa yametoa taarifa yakisema kuwa, Msikiti wa al Aqsa ni sehemu ya imani na itikadi za Waislamu na kwamba makundi ya mapambano ya Palestina kamwe hayatafumbia jicho hata shibri moja ya ardhi ya Quds na Msikiti wa al Aqsa.