Jun 01, 2016 07:02 UTC
  • Bahrain yasisitiza kuwanyonga wanaharakati 3 wa Kishia

Mahakama ya Rufaa ya Bahrain imekataa kutengua hukumu ya kunyongwa wanaharakati watatu wa Kiislamu wa madhehebu ya Shia.

Katika hukumu iliyotolewa jana Jumanne na koti hiyo, wanaharakati hao wanatuhumiwa kuhusika na mauaji ya maafisa watatu wa polisi katika kijiji cha Diah, katika hujuma ya bomu ya Machi mwaka 2014.

Mbali na kuidhinisha hukumu hiyo ya kunyongwa, Mahakama ya Rufaa ya utawala wa Manama imeidhinisha kifungo cha maisha jela, kwa vijana sita wanaodaiwa kuwashambulia maafisa usalama katika nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi. Kadhalika jana Jumanne mahakama moja nchini Bahrain iliwahukumu wanaharakati saba kifungo cha maisha jela, huku wengine watatu wakihukumiwa kifungo cha miaka 15 jela kwa madai ya kufadhili na kuunga mkono kundi la kigaidi.

Chama kikuu cha upinzani nchini humo cha al-Wefaq karibuni hivi kilitoa ripoti iliyosema kuwa, vyombo vya usalama vya Bahrain vimekamata watu 1,765 wakiwemo watoto wadogo 120 tokea mwaka jana 2015 hadi sasa, kwa lengo la kukandamiza maandamano ya amani ya wananchi wanaopinga dhulma za utawala wa Manama. Wananchi wa Bahrain wamekuwa wakifanya maandamano tokeo Februari mwaka 2011, kushinikiza kung'atuka uongozini utawala wa kifalme wa Aal-Khalifa.

Tags