Kuendelea mashambulizi ya kigaidi Afghanistan na majukumu ya Taliban
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i82844-kuendelea_mashambulizi_ya_kigaidi_afghanistan_na_majukumu_ya_taliban
Milipuko ya kigaidi iliyotokea hivi karibuni katika miji minne ya Afganistan baada ya kipindi kifupi cha utulivu wa kiwango fulani, imezusha mjadala mkubwa katika duru za kisasa na kiusalama. Kundi la kigadi la Daesh limetangaza kuhusika na milipuko hiyo ya umwagaji damu iliyouwa makumi ya watu na kujeruhi wengine wengi.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 24, 2022 02:29 UTC
  • Kuendelea mashambulizi ya kigaidi Afghanistan na majukumu ya Taliban

Milipuko ya kigaidi iliyotokea hivi karibuni katika miji minne ya Afganistan baada ya kipindi kifupi cha utulivu wa kiwango fulani, imezusha mjadala mkubwa katika duru za kisasa na kiusalama. Kundi la kigadi la Daesh limetangaza kuhusika na milipuko hiyo ya umwagaji damu iliyouwa makumi ya watu na kujeruhi wengine wengi.

Kuna nukta kadhaa hapa za kuzingatia na muhimu kuhusu mashambulizi ya kigaidi yanayofanyika huko Afghanistan yakiwemo mauaji na milipuko iliyoongezeka sana baada ya kundi la wanamgambo wa Taliban kushika tena hatamu za uongozi wa nchi mwezi Agosti mwaka jana. Mosi ni kuwa, kundi la Taliban liliwaahidi wananchi wa Afghanistan kwamba litawadhaminia usalama wao. Pili ni kuwa, kundi hilo limekuwa likidai mara kwa mara kwamba kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) halina nguvu wala uwezo wa kuhatarisha usalama wa Afghanistan, na kwamba limefanikiwa kulisambaratisha kundi hilo. Tatu ni kuwa, mashambulizi hayo ya kigaidi yanafanyika kwa mpangilio maalumu na yanaelekezwa katika maeneo makhsusi ambayo hayana usalama wa kutosha.  

Magaidi wa Daesh huko Afghanistan 

Pir Muhammad Mollazehi mchambuzi wa masuala ya Afghanistan anasema kuhusiana na suala hili kwamba: Mashambulizi ya kigaidi huko Afghanistan yamelenga zaidi jamii ya Waislamu wa madhehebu ya Shia katika maeneo mbalimbali ambayo hayana usalama na ulinzi wa kutosha; huku kundi la Taliban likilaani tu mashambulizi hayo kwa maneno kana kwamba halihusiki kivyovyote na hali hiyo.   

Kama walivyoeleza viongozi wa serikali ya zamani ya Afghanistan kwamba zaidi ya makundi ishirini ya kigaidi yalikuwa yakifanya hujuma nchini humo, hivi sasa pia si jambo lililo mbali kuhusika makundi mbalimbali katika mashambulizi sasa ya kigaidi. Jambo muhimu ni kuwa, sisitizo la Taliban kwamba inawajibika kulinda usalama wa wananchi wa Afghanistan ni madai matupu; hasa ikizingatiwa kuwa kundi hilo linajua na kuelewa kikamilifu mbinu mbalimbali za ugaidi na linao uwezo wa kuzuia mashambulizi ya kigaidi huko Afghanistan kwa kuandaa mikakati sahihi.  

Ali Khazai, mchambuzi wa masuala ya kisiasa anasema kuhusu hilo kwamba: Baada ya kuingia madarakani kwa mara nyingine tena huko Afghanistan, kundi la Taliban si tu limeshindwa kutatua matatizo ya Waafghani bali pia linadhihirisha kutokuwa na uwezo na kushindwa kuwadhaminia usalama  raia hao. Milipuko ya kigaidi inaficha kufeli Taliban katika maeneo mengine na wakati huo huo inalifanya kundi hilo kutumia masuala ya usalama kama kisingizio cha kubana anga ya jamii ya Afghanistan. 

Ala kulli hal, milipuko ya kigaidi iliyolenga maeneo matakatifu ikiwemo misikiti, ni ishara ya harakati zilizoratibiwa kwa lengo la kuibua vita vya kimadhehebu nchini Afghanistan. Wakati huo huo, hatua ya Taliban ya kupuuza kuunda serikali jumuishi na ya kitaifa nchini humo inaandaa mazingira ya kupingwa mienendo na maamuzi ya kundi hilo katika jamii ya nchi hiyo yenye kaumu na makabila tofauti. Hali hii pia inatatiza juhudi za kupeleka misaada ya kimataifa nchini Afghanistan na kuweka alama kubwa ya kuuliza kuhusu uwajibikaji wa Taliban katika sekta ya kulinda usalama wa watu wa Afghanistan. 

Msikiti mkongwe na mkubwa zaidi wa Washia huko Mazar- Sharif ulioshambuliwa na magaidi wa Daesh