Indhari kuhusu hali mbaya ya kibinadamu Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i83330-indhari_kuhusu_hali_mbaya_ya_kibinadamu_afghanistan
Ofisi ya Mkaguzi Mkuu Maalumu wa Marekani kwa ajili ya ujenzi mpya wa Afghanistan (SIGAR) imetahadharisha kuhusu taathira za hali mbaya ya kibinadamu nchini humo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 07, 2022 01:18 UTC
  • Indhari kuhusu hali mbaya ya kibinadamu Afghanistan

Ofisi ya Mkaguzi Mkuu Maalumu wa Marekani kwa ajili ya ujenzi mpya wa Afghanistan (SIGAR) imetahadharisha kuhusu taathira za hali mbaya ya kibinadamu nchini humo.

SIGAR imeeleza katika ripoti yake ya 55 kuhusu Afghanistan kuwa, zaidi ya watu milioni 24 na 400,000 wanahitaji misaada ya kibinadamu nchini humo. Japokuwa ripoti hiyo inasema kuwa, tangu kundi la Taliban lilishike tena hatamu za uongozi nchini Afghanistan mwezi Agosti mwaka jana idadi ya watu wanaohitaji misaada ya kibinadamu imeongezeka na kufika karibu milioni 6 huku wasio na ajira ikiwa karibu milioni moja, lakini nukta yenye umuhimu hapa kwamba, sababu na chanzo cha kuibuka matatizo makubwa ya kiuchumi na kijamii yanayoshuhudiwa sasa nchini Afghanistan mbali na vita vya ndani na uvamizi wa nchi ajinabi hususan katika miongo miwili iliyopita ambavyo vimeathiri vibaya na pakubwa hali ya nchi hiyo.  

Uvamizi wa wanajeshi wa Marekani, Afghanistan 

Pir Muhammad Mullazehi mchambuzi wa masuala ya Afghanistan anasema kuhusiana na hili kwamba: Mwaka 2001 Marekani iliivamia na kuikalii kwa mabavu Afghanistan kwa kauli mbiu ya "kuasisi nchi iiyokamilika, salama na yenye maisha bora kwa raia wake (utopia)." Katika miongo hiyo miwili si tu kuwa hakushuhudiwa unafuu wala maisha bora wa watu wa Afghanistan, bali pia hali imekuwa mbaya na ngumu zaidi. Ukweli ni kuwa, taasisi za Marekani haziwezi kuashiria hali hiyo ya mashaka na masaibu iliyowakumbwa watu wa Afghanistan kwa miongo miwili ya ya uvamizi wa Marekani na washirika wake wa Kimagharibi.  

Pamoja na hayo, kundi la Taliban linaloongoza Afghanistan linatambua vyema kuwa, halipasi kupuuza hali mbaya ya kiuchumi, kimaisha na ukosefu wa huduma za matibabu ya raia wa nchi hiyo. Kundi hilo ambalo linajifakharisha kwa hatua yake ya kuvifukuza Afghanistan vikosi vamizi vya nchi ajinabi, haliwezi kupatia ufumbuzi wa hali mbaya  ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ya nchi hiyo madhali linaendelea kung'ang'ania siaza zake za kuongoza nchi kiimla na peke yake. Hii ni kwa sababu, Afghanistan ni nchi yenye mchanganyiko wa makabila, madhehebu na kaumu tofauti; na tajiriba ya historia kuhusu matukio ya Afghanistan hasa wakati wa utawala wa muongo wa 90 wa kundi la wanamgambo wa Taliban, inaonyesha kuwa hatua ya kundi moja kuhodhi madaraka ya nchi haikufankiwa na kinyume chake, imekuwa ikiitumbukiza Afghanistan katika machafuko ya mara kwa mara na hali ya mchafukoge. 

Serikali ya Taliban 

Ali Vahedi mchambuzi wa masuala ya Afghanistan anatoa maoni yake akisema: Taliban haipasi kukariri makosa ya huko nyuma. Wananchi wa Afghanistan wanaitambua Taliban ya leo kuwa tofauti na ile ya muongo mmoja uliopita; na kundi hilo pia linapasa kuishirikisha mirengo yote ya kikabila na kisiasa chini ya anwani ya umoja wa kitaifa kwa ajili ya kuyapatia ufumbuzi matatizo ya Afghanistan.  

Ala kulli hal, ripoti zilizochapishwa kuhusu hali ya kiuchumi, umaskini, ukosefu wa ajira na hata tatizo la madawa ya kulevya huko Afghanistan zinatia wasiwasi mkubwa. Hasa ikizingatiwa kuwa, utumiaji wa mihadarati inayotengenezwa viwandani umeongezeka sana miongoni mwa watu wa nchi hiyo. Kwa msingi huo, kundi la Taliban linapasa kutumia suala la kuondoka vikosi wanajeshi vamizi wa Marekani huko Afghanistan kama fursa ya kihistoria kwa ajili ya kutatua matatizo na masaibu mbalimbali ya raia wa nchi hiyo kupitia njia ya kuimarisha umoja wa kitaifa kwa kuunda serikali jumuishi nchini humo.